Dalglish avutiwa na kifaa kipya Suarez

Meneja wa Liverpool Kenny Dalglish amebainisha mshambuliaji mpya Luis Suarez hajafanya mazoezi na wenzake na alifanikiwa kufunga bao la pili, wakati Liverpool walipowalaza Stoke 2-0.

Image caption Luis Suarez

"Hakupata hata nafasi ya kufanya mazoezi na wenzake, kutokana na urasimu wa kiutawala ambao baadae ilibidi ukamilishwe," alisema Dalglish baada ya mechi ya Jumatano.

"Atakapoanza mazoezi rasmi na wenzake nadhani tunaweza kuona kiwango cha juu cha Suarez.

Dalglish aliongeza: "Alijitahidi sana na akishirikiana na Dirk Kuyt walikuwa tishio katika ngome ya Stoke."

Suarez aliyenunuliwa kwa paundi milioni 22.7 kutoka klabu ya Ajax alifunga bao hilo la pili baada ya kumchanganya mlinda mlango Asmir Begovic na kuachia mkwaju uliomgonga mlinzi wa Stoke Andy Wilkinson na kuingia wavuni.

Bao hilo la Suarez lilipatikana dakika 16 baada ya kuingizwa akiwa mchezaji wa akiba, kabla bao la kuongoza la Raul Meireles, matokeo yaliyoisadia Liverpool kunawiri hata baada ya kuondokewa na mshambuliaji wake hatari Fernando Torres aliyehamia Chelsea kwa gharama za paundi milioni 50.