Garry Neville kubakia Man U kwa muda

Gary Neville, aliyestaafu kucheza soka siku ya Alhamisi, bado ataendelea kubakia katika klabu ya Manchester United kwa majukumu ambayo si rasmi hadi wakati wa majira ya joto.

Image caption Garry Neville

Mlinzi huyo wa kulia mwenye umri wa miaka 35, anahusishwa huenda kupatiwa ajira ya uchambuzi wa soka katika kituo cha televisheni cha Sky Sports ama ajira ya kudumu huko Old Trafford.

Lakini Neville amesema atafanya kazi na klabu yake ili apate cheti chake cha ukocha kabla hajaamua mustakabali wake kwa siku zijazo.

"Kwa wakati huu mawazo yangu yapo kwenye ukocha au utawala wa soka," aliongeza.

"Nimekuwa nikifanya kazi na klabu ya soka kila siku kwa miaka 20. Kwa hakika ninachotaka ni kujaribu kuendeleza ushirikiano wangu na klabu hii, hata kama nikiwa shabiki tu.

Neville alianza kucheza soka katika klabu ya Manchester United mwezi wa Septemba mwaka 1992 katika mechi dhidi ya Torpedo Moscow, kuwania kombe la Uefa na alicheza mechi yake ya 602 kwa mara ya mwisho wakati Manchester United walipoishinda West Brom mabao 2-1 siku ya mwaka mpya.