Mabao mengi yafungwa Ligi ya England

Arsenal wakiwa wanaongoza mabao 4-0 dhidi ya Newcastle hadi kipindi cha kwanza, walishindwa kulinda lango lao kipindi cha pili na Newcastle wakamudu kurejesha mabao yote manne, na kusababisha timu hizo zigawane pointi.

Image caption Ligi Kuu ya England

Arsenal ndio walikuwa wa kwanza kufunga dakika ya kwanza tu kwa bao lililofungwa na Theo Walcott.

Kipindi cha kwanza kilikuwa cha Arsenal kwani dakika mbili baadae Johan Djourou akaandika bao la pili, kabla ya Robin van Parsie kufunga bao la tatu katika dakika ya 10 na la nne katika dakika ya 26.

Katika mchezo huo Abuu Diaby wa Arsenal alitolewa nje kwa kadi nyekundu.

Kwa matokeo hayo Arsenal bado wanashikilia nafasi ya pili wakiwa na pointi 50 na Newcastle wapo nafasi ya 10 na pinti 31.

Katika mchezo mwengine Evertin waliutumia vilivyo uwanja wa nyumbani baada ya kuwalaza Blackpool mabao 5-3.

Louis Saha katika mchezo huo alifunga mabao manne peke yake.

Everton wamefikisha pointi 30 wakiwa nafasi ya 13.

Wigan nao kwa ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Blackburn, wamefanikiwa angalao kwa muda kujinasua kutoka eneo la hatari la kuteremka daraja.

Sasa Wigan wapo nafasi ya 17 wakiwa na pointi 26.

Manchester City kwa mabao matatu yaliyofungwa na Carlos Tevez dhidi ya West Brom, wamezidi kujiimarishas nafasi ya tatu kwa kupata pointi 49.

Aston Villa katika pambano lao dhidi ya Fulham walilazimishwa sare ya mabao 2-2.

Tottenham nao waliutumia vizuri uwanja wa nyumbani baada ya kuwalaza Bolton mabao 2-1 na kuendelea kushikilia nafasi ya tano wakiwa na pointi 44.

Pambano la mapema lililochezwa mchana, Stoke City walifanikiwa kujiuliza na kufanikiwa kuwalaza Sunderland mabao 3-2.