United yagonga ukuta

Mbio za Manchester United kwenda bila kufungwa zimefikia ukingoni baada ya kuzabwa mabao 2-1 na Wolverhampton.

United ndio ilikuwa ya kwanza kuliona lango la Wolves katika dakika ya tatu, kupitia Nani.

Image caption Chungu ya kufungwa... Alex Ferguson

Hata hivyo George Elokobi, ambaye alikuwa nyota wa mchezo huo, alisawazisha bao hilo katika dakika ya 10.

Dakika tano kabla ya mapumziko, Kevin Doyle alipachika bao la ushindi la wenyeji.

United walipigana kufa na kupona kujaribu kutafuta japo sare, lakini ngome ya Wolves ilikaa imara na kuwanyima vijana wa Sir Alex Ferguson kuendeleza wimbi lao la kutopoteza mchezo msimu huu.

United inaendelea kusalia kileleni, huku Wolves wakipata pointi tatu muhimu, ingawa nao wamesalia mkiani katika msimamo wa ligi.