Roberto Di Matteo apumzishwa West Brom

Meneja wa West Brom Roberto Di Matteo amepumzisha kazi zake na amepewa likizo mara moja, huku masuala yake yakishughulikiwa.

Image caption Roberto Di Mateo

West Brom walifungwa 3-0 na Manchester City siku ya Jumamosi na klabu hiyo tayari imepoteza michezo 13 kati ya 18 ikiwa ni moja ya sababu ya uamuzi huo.

Mwenyekiti wa West Brom, Jeremy Peace amesema:"Huu ni uamuzi mgumu."

"Lakini sisi kwenye bodi, tunaamini ni sahihi kuipatia nafasi klabu hii ya uwezekano wa kuendelea kusalia katika Ligi Kuu."

Di Matteo, kiungo wa zamani wa Chelsea, alichukua hatamu za kuifundisha West Brom mwezi wa Juni mwaka 2009 na akafanikiwa kuipandisha timu hiyo msimu uliopita hadi Ligi Kuu.

Timu hiyo katika mchezo wake wa ufunguzi wa ligi msimu huu, ilichabangwa mabao 6-0 na Chelsea, lakini baadae wakaamka na wakapoteza mechi mbili katika tisa za awali, ikiwemo ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Arsenal na sare ya 2-2 na Manchester United.

West Brom kwa muda ilifanikiwa kuwemo katika timu nne za juu baada ya kuilaza Fulham mwezi wa Oktoba, lakini matokeo yaliyofuatia yalikuwa mabaya na kuididimiza timu hiyo katika miezi ya karibuni na kwa sasa wapo pointi mbili tu kutoka mstari wa kuteremka daraja.

Msaidizi wa Di Matteo, Eddie Newton na mkuu wa sayansi ya michezo Ade Mafe, pia wameondoka katika klabu hiyo na kocha wa timu ya kwanza Michael Appleton ameondolewa kwa muda, huku klabu hiyo ikikabiliwa na mechi dhidi ya wenzao wanaotapatapa kushuka daraja, West Ham na Wolves.