Algeria yahimiza mabadiliko

Mjumbe maalum wa chama kinachotawala nchini Algeria amehimiza yafanyike mageuzi serikalini, ishara kwamba viongozi wa nchi hiyo wana wasiwasi kuhusu vuguvugu la maandamano katika nchi jirani za Tunisia na Misri litasambaa hadi Algeria.

Image caption Mabadiliko.... Rais Abdelaziz Bouteflika

Zohra Drif Bitat, ambae ni Makamu Rais wa baraza la wazee la bunge alishutumu vikali serikali kupitia kituo cha radio ya taifa akisema licha ya utajiri mkubwa wa mafuta na gesi wananchi wa kawaida bado wanasumbuliwa na hali ya umasikini.

Alisema ni makosa kwa wanasiasa wale wale kukabiliana na matatizo hayo, na kuhimiza kile alichokieleza damu mpya "iletwe ndani ya serikali".

Hizi ni shutuma zisizo za kawaida kutoka kigogo wa chama kinachotawala na ni ishara ya jinsi viongozi wa Algeria wanavyotazama vuguvugu la maandamano katika nchi za Tunisia na Misri.

Image caption Bouteflika

Wiki iliyopita Rais , Abdelaziz Bouteflika, wa Algeria alihidi kuondoa hali ya amri ya hali ya hatari ambayo imeendelea kwa muda wa miaka 19, kuweka ajira zaidi na kuruhusu haki zaidi za kidemokrasia.

Lakini mkutano uliopangwa na vikundi vya upinzani mjini Algiers siku ya Jumaamosi umepigwa marufuku.

Waandaaji wa maandamano hayo wanasema watakiuka amri hiyo na kuandamana katika mji mkuu.