Mishahara yaongezwa Misri

Baraza jipya la mawaziri nchini Misri limetangaza nyogeza ya mshahara kwa wafanyakazi wa serikali, kwa mara ya kwanza tangu kuanza vuguvugu la maandamano wiki mbili zilizopita.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waandamanaji Misri

Kuna wafayakazi millioni sita katika sekta ya umma nchini Misri.

Mnamo siku za nyuma wengi wao walikuwa wafuasi wakubwa wa serikali lakini katika miaka ya hivi karibuni mishahara ya chini na bei ghali za vitu vimesababisha manun'guniko mengi.

Wizi wa kura

Na sasa baada ya takriban wiki mbili za machafuko, juhudi zinaendelea kujaribu kuwavutia kuiunga mkono serikali kwa kuwapa nyongeza ya asilimia 15 kwa mshahara na malipo ya uzeeni,kuanzia mwezi wa Aprili.

Hapo awali baraza la mawaziri pia lilitoa ahadi mpya za kuchunguza vitendo vya rushwa serikalini na wizi wa kura.

Na ikatangaza kuwa mmojawapo wa vijana waliotayarisha maandamano hayo ambaye ni meneja wa huduma ya tovuti ya Google ataachiliwa.

Lakini hatua zote hizi hazijazuia ari ya waandamanaji kuendelea maandamano yao katika uwanja wa Tahrir Square - na kuendelea kudai Rais Mubarak aondoke.