Fifa yazitupa rufaa za Adamu na Temarii

Fifa imetupilia mbali rufaa za wajumbe wake wawili wa zamani waliosimamishwa baada ya tuhuma za rushwa wakati wa mchakato wa kutafuta nchi zitakazoandaa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022 .

Image caption Adamu na Temarii

Baada ya mkutano wa siku mbili, Kamati ya Fifa ya Rufaa, imekubaliana na uamuzi wa wa Kamati yake ya Maadili uliochukuliwa mwezi Novemba.

Amos Adamu kutoka Nigeria mwenye umri wa miaka 58, ni lazima atumikie adhabu ya miaka mitatu, ingawa amethibitisha atapeleka shauri lake mbele ya mahakama inayoshughulikia kesi za michezo.

Na hukumu dhidi ya Reynald Temarii raia wa Tahiti, itaendelea kwa kipindi cha mieizi 12 ijayo.

Wajumbe hao walifanyiwa uchunguzi na Fifa baada ya gazeti la Sunday Times kubainsha tuhuma kwamba wapo tayari kuuza kura zao kwa nchi zilizokuwa katika kinyan'ganyiro cha kuwania kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022 .

Wote wawili walizuiwa kushiriki katika upigaji kura, ambapo Urusi na Qatar zilishinda.

Adamu, ambaye ana matumaini ya kuwania tena nafasi yake katika Kamati Kuu ya Fifa, wakati Afrika itakapofanya uchaguzi wake baadae mwezi huu, amesema: "Nimevunjika moyo sana kutokana na uchunguzi wa Kamati ya Rufaa ya Fifa."

Shirikisho la Soka barani Afrika, litafanya mkutano wake mkuu wa mwaka tarehe 23 mwezi wa Februari mjini Khartoum, Sudan, ambapo itawachagua wajumbe wake wawili kati ya wanne katika Fifa.