Sudan Kusini kuthibitisha mgawanyiko

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Watu wakisherehekea wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya awali

Matokeo rasmi ya kura ya maoni iliyofanyika Sudan kusini juu ya kujitenga unatarajiwa kutangazwa.

Matokeo ya awali yanayoonyesha takriban asilimia 99 ikiunga mkono kugawanywa kwa nchi kubwa kuliko zote Afrika unatarajiwa kuthibitishwa.

Kura ya maoni ya Januari ulikubaliwa kama sehemu ya makubaliano ya amani ya mwaka 2005 ya kumaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baina ya kusini na kaskazini yaliyodumu kwa miongo miwili.

Licha ya kura hiyo kuwa ya amani, wasiwasi unaendelea kuongezeka katika baadhi ya maeneo ya mpakani yenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Takriban watu 50 waliuawa mwishoni mwa juma katika mapigano baina ya askari katika jimbo la Upper Nile kusini mwa Sudan.

Mapigano hayo yalitokea baina ya askari wa kaskazini wakigombania nani atamiliki mizinga mikubwa baada ya silaha hizo kuhamishwa kaskazini kwenye mpaka mpya.

Mapigano hayo yalianza mwishoni mwa wiki iliyopita katika mji mkuu wa Malakal, na kuenea kwenye miji ya Paloich na Melut mwishoni mwa juma.