Ancelotti asisitiza Torres ataimarika

Meneja wa Chelsea, Carlo Ancelotti, anaamini mchezaji mwenye thamani ya paundi milioni 50 Fernando Torres, anahitaji muda kuzoea kabla hajaanza kuonyesha makali.

Image caption Fernando Torres akikabiliana na Jamie Carragher

Torres kwa kiasi kikubwa hakuonesha makali katika mechi yake ya kwanza tangu alipojiunga na Chelsea, ambapo timu yake ya zamani ya Liverpool iliilaza Chelsea bao 1-0 siku ya Jumapili na alibadilishwa katika dakika ya 66.

Lakini Ancelotti alisisitiza mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26, hana muda mrefu kabla ya kuanza kuvyatua makombora na kufunga, ili kuhalalisha thamani yake ambapo amevunja rekodi ya Uingereza kwa kununuliwa kwa pesa nyingi.

"Hatuna budi kumpatia Fernando muda wa kuzoea, lakini natumai atazoea haraka," alisema Ancelotti.

Torres, amekuwa mchezaji ghali zaidi katika historia ya soka ya Uingereza wakati wa dirisha dogo la usajili tarehe 31 mwezi wa Januari, alikuwa na kibarua cha kukabiliana na kelele za kumkashifu kutoka kwa mashabiki wa Liverpool, wakati akicheza mechi yake ya kwanza akiwa amevalia fulana ya Chelsea.

"Nilimtoa baada ya dakika 66 na ilikuwa ni wiki yenye hekaheka nyingi, ilikuwa jambo jema kwake kupumzika," aliongeza Ancelotti.

"Fernando ana uzoefu, anajiamini na hakuwa na tatizo lolote kabla ya mechi.

"Alikuwa na shauku kubwa ya kucheza na si vinginevyo."

Ancelotti alimchezesha Torres katika safu ya ushambuliaji pamoja na Didier Drogba, huku mshambuliaji mwengine Nicolas Anelka akicheza nyuma yao kidogo.

Hata hivyo, Chelsea mara chache sana iliisumbua Liverpool, iliyokuwa ikicheza kwa nidhamu na kwa mpangilio, na kushinda kwa bao la Raul Meireles, akifunga bao lake la nne katika mechi tano zilizopita.