Chama cha Ben Ali chasimamishwa

Chama cha RCD ambacho kilikuwa chama tawala nchini Tunisia kimesimamishwa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waandamanaji wamebeba bendera ya Tunisia

Wizara ya mambo ya ndani nchini humo imetangaza chama hicho cha Ben Ali, kimesimamishwa na ofisi zake kufungwa.

Taarifa iliyotolewa kwenye televisheni ya taifa ilisema chama hicho kimepigwa marufuku na wanasubiri uamuzi iwapo chama hicho kitavunjwa.

Taarifa hiyo imetolewa wiki tatu baada ya waandamanaji kumlazimisha Rais Zine al-Abidine Ben kuachia madaraka.

Hii ni baada ya ghasia kutokea mwishoni mwa juma ambapo watu watatu waliuwawa.

Polisi waliwafyatulia risasi waandamanaji katika mji wa Kef, Jumamosi, na kuwaua watu wawili.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Waandamanaji nchini Tunisia

Waandishi wa habari wamesema kuwa iwapo chama hicho kitavunjwa, itakuwa hatua kubwa tangu Ben Ali kuikimbia nchi hiyo.

Chama cha RCD ndicho chama kilichomweka Ben Ali madarakani.

Ben Ali alikimbilia nchi ya Saudi Arabia tarehe Januari 12 baada ya mwezi moja wa maandamano.

Umoja wa Mataifa umekadiria kuwa watu wapatao 200 walifariki dunia katika vurugu hizo.

Hivi sasa kuna serikali ya mpito ambayo inaongozwa na Waziri Mkuu Mohammed Ghannouchi huku uchaguzi ukitazamiwa kufanyika katika kipindi cha miezi sita au saba.

Maandamano ya Tunisia yameleta mtafaruku katika nchi za Uarabuni na hata kusababisha maandamano nchini Misri.