Obafemi Martins apata kibali Birmingham

Mshambuliaji wa Nigeria, Obafemi Martins hatimaye amerejea Uingereza baada ya kufanikiwa kupata kibali cha kuingia nchini, kitajkachomuwezesha kuichezea Birmingham City.

Image caption Obafemi Martins

Martins mwenye umri wa miaka 26 alijiunga na 'The Blues' kwa mkopo tangu mwezi wa Januari akitokea klabu ya Rubin Kazan ya Urusi, lakini kikwazo kilikuwa ni viza iliyomzuia kucheza.

Taarifa iliyotolewa kupitia mtandao wa Birmingham City, imesema Martins alipata kibali na atacheza mchezo wa Jumamosi dhidi ya Stoke City.

Mechi hiyo itamfanya Martins kurejea tena katika Ligi Kuu ya Soka ya England, akiwa ameichezea Newcastle United kwa miaka mitatu na kufunga jumla ya mabao 39 katika michezo 105.

Kwa mujibu wa kocha wa Birmingham Alex McLeish, mashabiki watamkubali haraka Martins.

"Yeye ni mchezaji mwenye nguvu na mikwaju mikali na unaweza kumfananisha na Christian Benitez, lakini ana uzoefu zaidi," alisema McLeish.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Nigeria, alishawahi kuchezea klabu ya Inter Milan ya Italia kwenye ligi ya nchi hiyo maarufu Serie A na vilevile Wolfsburg ya Ujerumani katika Bundesliga.