Jeshi lajaribu kuondoa watu Tahrir

Kuna mvutano mkali katika eneo la Tahrir mjini Cairo nchini Misri, kutokana na waandamanaji walioweka kambi hapo kwa muda wa siku 20, wakizuia juhudi za jeshi kuwaondoa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Polisi wakiwashawishi waandamanaji kuondoka

Maelfu ya watu zaidi wameelekea katika eneo hilo la wazi, ambalo ndio kitovu cha maandamano yaliyosababisha kuondoka kwa Rais Hosni Mubarak siku ya Ijumaa.

Jeshi linaonekana kutojua jinsi ya kukabiliana na kundi jipya la watu wanaofika katika eneo hilo, anasema mwandishi wetu Jon Leyne akiwa katika eneo la tukio.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Polisi wa kijeshi (MP) wakikabiliana na waandamanaji

Mkuu wa polisi wa kijeshi (MP) ametaka mahema yote katika eneo hilo kuondolewa.

"Hatutaki kuona waandamanaji katika eneo hilo baada ya leo," amesema Mohamed Ibrahim Moustafa Ali, mkuu wa polisi wa kijeshi.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Hosni Mubarak

Rais Obama wa Marekani, mapema alifurahia tamko la jeshi hilo la kuahidi kufanya mchakato kuelekea katika utawala wa kiraia.

Jeshi hili limesisitiza kuzingatia makubaliano yote ya kimataifa.

Hasira zilizuka siku ya Jumapili asubuhi, baada ya waandamanaji kuona mamia ya polisi - ambao walipoteza umaarufu kwa kutumia nguvu wakati maandamano yanaanza - kuingia katika eneo hilo.