Misri washerekea kuondoka kwa Mubarak

Maelfu ya wananchi wa Misri bado wametapakaa katika eneo la wazi la Tahrir mjini Cairo, siku moja baada ya kujiuzulu kwa Rais Hosni Mubarak.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waandamanaji wamekesha Tahrir

Katika hali ya sherehe, watu wameanza kusafisha eneo hilo la wazi, huku wanajeshi wakiondoa vizuizi, ingawa vifaru bado vimesalia.

Baada ya miaka 30 madarakani, Bw Mubarak alilazimishwa kuondoka madarakani kufuatia siku 18 za maandamano ya kupinga serikali.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Sherehe baada ya Mubaraka kutangaza kuondoka

Nchi sasa iko mikononi mwa jeshi.

Rais wa Marekani Barak Obama ameita nchi ya Misri kuwa yenye kuhamasisha, lakini amesema lazima nchi hiyo ielekee katika utawala wa kiraia na wa kidemokrasia.

Rais huyo amemtuma Adm Mike Mullen, mwenyekiti wa wakuu wa jeshi la Marekani, kwenda Jordan na Israel kujadili hali ya mabadiliko ya Misri.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waandamanaji Tahrir

Muda mfupi kabla ya tangazo la kujiuzulu, Bw Mubarak aliondoka mjini Cairo kuelekea mji wa Sharm el-Sheikh uliopo kwenye pwani ya bahari ya Sham, ambapo ana makazi yake mengine.

Mandamano ya kupinga serikali yaliyoanza Januari 25, yalichochewa na kuenea kwa hali ya mashaka nchini Misri, kutokana na ukosefu wa ajira, umasikini na ufisadi.