FA yaonya wachezaji na kashfa mitandaoni

Wachezaji wa soka huenda wakashtakiwa kutokana kuandika na kutuma katika mtandao ya kijamii kashfa dhidi ya watu wengine, Chama cha Soka cha England -FA- kimeonya.

Haki miliki ya picha 1
Image caption Ryan Babel

FA kimefafanua msimamo wake katika taarifa rasmi waliyotuma kupitia mtandao wake siku ya Jumamosi.

Chama hicho cha Soka, kilimpiga faini winga wa zamani wa Liverpool, Ryan Babel mwezi wa Januari, kutokana na maoni yake aliyotuma katika mtandao wa Twitter, dhidi ya mwamuzi Howard Webb.

Image caption Howard Webb

Babel ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Hoffenheim ya Ujerumani, alipigwa faini ya paundi 10,000.

Taarifa ya FA imesema: "Maoni yanayotolewa katika mitandao ya kijamii, huenda yakachukuliwa ni maoni ya hadharani, maoni yoyote ambayo yanayoonekana kukashifu, yanayoufanya mchezo wa soka ukose heshima au yanayotishia, kutukana na kukashifu huenda hatua za nidhamu zikachukuliwa.

"Maoni ambayo yanamlenga mtu binafsi au huenda yamepangwa kama shambulio, kutumia lugha ya kashfa au yenye kumlenga mtu kwa kumtishia moja kwa moja au kwa kutumia lugha ya kupindapinda, huenda yakachukuliwa ni utovu wa nidhamu na kashfa.

"Watu wote wanatakiwa kutenda kwa kuuheshimu mchezo wa soka wakati wote na hawana budi kuelewa jambo hili wakati wanapotumia mitandao ya kijamii.

"Zaidi ya hapo, wote wanakumbushwa kutuma kwenye mitandao ya kijamii kitu wanachoamini kitaonekana kwa idadi fulani ya watu waliokusudiwa, bado huenda ikaonekana ni jambo lililolengwa kwa jamii nzima na uangalifu unatakiwa uwepo kwa kuzingatia yale yaandikwayo na kutumwa katika mitandao hiyo.

"Kwa kuongezea, tungependa kuwakumbusha wote kwamba kuandika na kutuma katika mitandao ya kijamii, kunaweza pia kusababisha kufunguliwa kwa shauri mahakamani na wale watakaohisi wamechafuliwa heshima yao."

Hivi karibuni, kiungo wa timu ya taifa ya England na Arsenal Jack Wilshere, alituma katika mtandao wa Twitter, shutuma dhidi ya mwamuzi Phil Dowd, lakini hakuadhibiwa na FA.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Jack Wilshere

Wakati Wilshere kwa ufupi tu aliandika kuhusu "waamuzi wanaolegalega", Babel yeye alituma picha ya Webb akiwa amevaa fulana ya Manchester United, ikimaanisha mwamuzi huyo kwa makusudi alikuwa akiipendelea timu hiyo.