Wafanyakazi wa umma wagoma nchini Misri

Watumishi wa umma wanaogoma Misri Haki miliki ya picha AP
Image caption Watumishi wa umma wanaogoma Misri

Maelfu ya wafanyakazi wa umma nchini Misri, wameitisha maandamano ya kitaifa kupinga mazingira mabaya ya kazi na pia mishahara duni.

Wafanyakazi hao wamepuuza wito wa viongozi wa kijeshi nchini humo wa kusitisha maandamano hayo ambayo yameathiri uchumi wa taifa hilo kwa kiasi kikubwa.

Waandamanaji wapya wamefurika bustani ya Tahrir, baada ya wanajeshi kufanikiwa kuwatimua waandamanaji wengine waliokuwa wamepiga kambi katika bustani hiyo katika maandamano yaliyopelekea rais Hosni Mubarak.

Huku hayo yakijiri, utawala wa nchi hiyo umesema kura ya maoni kuhusu katiba mpya, nchini humo itaandiliwa katika kipindi cha miezi miwili ijayo na kwamba viongozi wa upinzani watajumuishwa katika serikali ya mpito.

Mataifa kadhaa barani ulaya yamethibitisha kupokea ombi kutoka kwa utawala wa kijeshi nchini Misri wa kuzuia mali inayomilikiwa na maafisa wakuu wa serikali iliyoondolewa madarakani, iliyoongozwa na Hosni Mubarrak.