'Nyumba za kujiua'

Picha ya binti aliyejiua huko Sendai Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Picha ya binti aliyejiua huko Sendai

Japan ni nchi yenye idadi ya watu wengi wanaojiua duniani na kwa wastani takriban watu 100 hujiangamiza kila siku.

Lakini katika maeneo ambapo matukio hayo hutokea huacha athari kubwa kwa familia zilizobaki.

Katika chumba chenye vikorokoro huko Sendai, hewa iliyojaa moshi wa sigara, mzazi huinama akiswali.

Akiwasha udi na kugonga kengele mbele ya madhabahu, kabati la mbao lenye mapambo.

Picha ya binti yake haiko pamoja na picha za mababu zake, bado iko kwenye kabati la vitabu.

Kuiweka hapo itakuwa ni ishara ya mwisho ya kukubali kwamba hayupo tena, na kwamba miaka miwili iliyopita alikuta mwili wa binti yake kwenye nyumba aliokuwa amepanga.

Alikuwa na miaka 22 tu na baba yake mpaka sasa ameshindwa kukubaliana na hali hiyo.

Alisema, "Nilipogundua kuwa kafariki dunia sikuweza kutembea na wala sikuweza kufikiri hata kidogo."

"Sikuamini kilichotokea. Niliamini hakuna Mungu katika dunia hii. Hicho ndicho ninachokumbuka tangu siku ile."

Ni baba, na aliyekuwa mke wake, na mama wa binti huyo, ndio wanaojua kuwa mtoto wao alizidisha kiasi cha dawa kuliko kinachotakiwa.

Ndugu wengine na marafiki hawakuwahi kuambiwa kuwa alijiua, kwahiyo hakutaka jina lake litajwe.

Haikuwa muda mrefu baada ya kifo cha binti huyo ambapo alipata mshtuko mwengine, mara hii barua kutoka kwa mwenye nyumba wake.

Anakumbuka, " Tulifanya mazishi yake mwisho wa mwezi Machi."

" Hati ya madai ya kodi kwa ajili ya kukarabati nyumba ililetwa mwezi Aprili, halafu ikatakiwa fidia kwa kodi ya mwezi Mei. Kwahiyo ilikuwa jambo moja baada ya jengine."

" Kitu pekee nilichokuwa naweza kufikiria ni mwanangu niliyempoteza. Kwahiyo nilipokuwa napata hati hizo, sikuwa na nia wala nguvu ya kujadili au kukataa."

Kwa jumla alilipa zaidi ya dola za kimarekani 30,000.

Matambiko ya kutakasa

Japan ina utamaduni wa kihistoria wa kujiua kama heshima. Lakini huku idadi ya waliojiua ikiongezeka, umma umezidi kuwa na wasiwasi.

Watu wachache watakubali kukodi nyumba ambapo mwanzo aliishi mtu aliyejiua. Kwahiyo aghlabu kifo cha mtu hufuatiwa na kudaiwa fedha.

Sachiko Tanaka ambaye aliunda shirika la kusaidia familia zilizopoteza watoto wao baada ya mwanawe binafsi wa kiume kujiua alisema, " Wako wengi."

"Mara nyingi ni fidia ya kukosa kodi za nyumba. Kiwango kikubwa kabisa kilikuwa dola za kimarekani 900,000. Madai yalikuwa kwamba jengo zima halikuwa na thamani tena kwasababu mtu mmoja alijiua humo ndani. Kwahiyo inabidi walipe ili kulijenga upya."

Familia nyingi nazo pia hutakiwa kulipa gharama kubwa kwa ajili ya matambiko ya mtakaso.

Shirika hilo linashughulikia malalamiko ya takriban watu 200 wanaodaiwa pesa chungu nzima na wenye nyumba wao waliowapangisha hivyo anatoa wito wa kufanya mabadiliko ya sheria.

Tayari mpaka sasa mawakala wa kupangisha nyumba wako makini kuwasaidia wafiwa.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Nyumba ambapo mtu alijiua, Japan

Yoshihiro Kanuma anacho kile anachokiita nyumba inayompa shida kubwa kuuza. Alishawishika kuichukua kutokana na imani yake ya madhehebu ya Buda.

Ni eneo la kawaida tu, lenye umri wa miaka kadhaa- ambapo kwa biashara za Japan huziita 3LDK;vyumba vitatu, ukumbi, chumba cha kulia na jiko, katika mji nje ya Tokyo.

Ziara hiyo huendelea mpaka kwenye chumba kikubwa, ambapo kwa mbele yake unaona shamba la mpunga, lakini mwisho wake lazima amwambie yeyote mwenye nia ya kununua kuwa mtu wa mwisho aliyepangisha alijinyonga.

Alisema, "Watu tisa miongoni mwa 10 husema sitaki kwa namna yeyote kuhusika na nyumba hiyo."

"Wajapani huweza kudhani kuwa nyumba ina nuksi. Japo nahisi wengine wanaona ni jambo la kishujaa kujiua, lakini kwa minajil ya nyumba watu hawaichukulii hivyo. Tunahisi nyumba haijatakasika na italeta huzuni. Binafsi nafikiri nyumba haihusiki kwa lolote lakini Wajapani wengi wanahisi hivyo."

Bw Kanuma amefanikiwa kuishawishi familia moja angalau kuonyesha nia ya kununua, japo ni nusu ya bei ya nyumba nyingine eneo hilo.

Tukirudi Sendai baba wa mfiwa amekaa kimya kwenye kiti chake, na kuwasha sigara nyingine.

Anakiri kuwa amebadilika ambapo anajitenga peke yake, na anasema hata yeye angependa afe.

Ukilinganisha na kumpoteza bintiye pesa si kitu, lakini kama ilivyo kwa Wajapani wengi si kwamba anateseka tu kwa kufiwa, lakini pia kwa matatizo ya kiuchumi.