Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Mwivi mwenye heshima

Mwizi mmoja nchini Marekani ametoa mpya ya aina yake, baada ya kwenda kufanya wizi huku akiwa na adabu kabisa.

Mara kadhaa mwizi huyo alikuwa akitumia neno tafadhali, na kumuita mtu anayemuibia 'sir', kuonesha heshima yake.

Image caption Tafadhali, nipatie pesa zote.. Hess akifanya wizi

Mwizi huyo mwenye umri wa miaka sitini na mitano alimshikia bastola muuza duka katika kituo kimoja cha mafuta, na kumuambua 'tafadhali' wakati akitaka kupewa fedha zilizokuwa kwenye droo la kuwekea fedha.

Baada ya kununua kikombe cha kahawa dukani hapo, mjini Seattle, Washington, na kulipia, kimya kimya alitoa bastola yake na kumuelekezea mwenye duka.

Akizungumza kwa taratibu akamwambia muuza duka, 'nifanyie msaada, hebu nipatie hizo fedha zote kwenye droo yako tafadhali'.

Mwenye duka alipouliza kulikoni, mwizi huyo Gregory Hess alimuambia 'nakuibia mzee' kwa adabu kabisa. Mwenye duka alipomuuliza kwa nini? Mwizi alijibu kwa heshima zote, 'kwa sababu nahitaji fedha', nina watoto wanaohitaji kula, naomba radhi sana kwa kufanya hivi' alisema mwizi huyo.

Mwenye duka alipojitolea kumpa dola arobaini, mwizi huyo kwa unyenyekevu alikataa na kuomba apewe fedha zote, ambazo zilikuwa kama dola mia tatu.

Baada ya kupewa alishukuru 'asante sana, nakushukuru, mambo yangu yakikaa sawa nitakulipa' alisema mwizi huyo.

Baadaye mwenye duka huyo John Henry alisema amewahi kuibiwa mara kadhaa, lakini hajawahi kuonea huruma mwizi kama alivyofanya wakati huu.

Mwizi huyo amekamatwa na atafikishwa mahakamani.

Wachawi kutozwa faini

Mwezi mmoja tangu mamlaka za Romania kuanza kuwatoza kodi wachawi, watabiri na wapiga ramli nchini humo wamelaani sheria mpya itakayowalazimu kulipa faini, iwapo utabiri wao hautakuwa wa kweli.

Haki miliki ya picha av.com
Image caption Malkia wa uchawi

Mwezi Januari mwaka huu serikali ilibadili sheria na kuwatambua rasmi wachawi, na kuwataka walipe kodi kwa kazi yao hiyo.

Hatua hiyo iliwakasirisha mno wapiga ramli hao kiasi cha kutishia kuitupia serikali uchawi mzito.

wiki iliyopita, muswada wa sheria umewasilishwa katika bunge la nchi hiyo kuwataka walipe faini, ikiwa utabiri wanaotoa kwa wateja usipotokea.

Mmoja wa wakuu wa masuala ya uchawi, Malkia wa uchawi Bratara Buzea amesema "Hawawezi kuwatupia lawama wachawi, wanatakiwa pia kutazama upande wa pili" amesema.

Mchawi huyo amesema atapigana kufa na kupona kuhakikisha muswada huo haupitishwi bungeni.

Malkia Bratara amesema wakati mwingine utabiri wao hautokei kama wanavyobashiri kwa kuwa wateja huwapa taarifa zisizo za kweli.

"Wengine hawasemi ukweli tarehe zao za kuzaliwa, au majina yao halisi, hiyo inasababisha dawa kutofanya kazi" amesema mwanaharakati huyo wa nguvu za giza.

Mtandao wa habari wa Scotsman.com unasema wakosoaji wanadai kuwa hatua hiyo ni ya kupoteza lengo kwa wananchi, kwani nchi hiyo ina matatizo mengi.

Wezi wakimbilia jela kujificha

Washukiwa wawili wa wizi nchini Colombia wamekamatwa, baada ya kukimbilia ndani ya gereza ili kujificha.

Shirika la habari la BBC limesema wezi hao walikuwa wakifukuzwa na polisi baada ya kufanya wizi katika mtaa mmoja wa mji mkuu wa nchi hiyo Bogota.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Angalia kabla ya kuruka...

Wezi hao walipanda juu ya paa la nyumba na kuanza kukimbia, wakiruka kutoka paa la nyumba moja kwenda jingine.

Waliendelea kufanya hivyo, paa hadi paa, na mara walifika kwenye ukuta wa gereza na, bila kujua wakarukia ndani yake.

Gereza hilo linaitwa La Picota, na ni gereza kubwa zaidi nchini Colombia. Mara baada ya kurukia ndani ya ukuta wa gereza, kengele za usalama zilianza kupiga kelele, na kusababishwa kukamatwa kirahisi kabisa.

Wezi hao wamefikishwa katika mamlaka za kisheria, na wanasubiri kuona kama watafunguliwa mashitaka.

Shirika la habari la BBC limesema iwapo watashitakiwa mahakamani na kukutwa na hatia, huenda wakapelekwa kutumikia kifungo chao katika gereza kuu la, La Picota.

Getto la masela.

Msichana mla sabuni

Haki miliki ya picha madnews
Image caption Tempestt Henderson

Msichana mmoja nchini Marekani anapatiwa matibabu kutokana na hali yake ya kupenda kula sabuni.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 19 Tempestt Henderson wa Florida, hula takriban miche mitano ya sabuni kwa wiki, na kulamba kiasi kikubwa tu cha sabuni ya unga.

Haki miliki ya picha madnews
Image caption Tamu...

Kwa mujibu wa madaktari, msichana huyo ana maradhi yajulikanayo kama PICA, ambayo huleta hamu ya kula vitu visivyo na virutubisho.

watu wanaoungua ugonjwa huo, hupenda kula vitu kama, vyuma, sarafu, betri, na hata miswaki.

Haki miliki ya picha madnews
Image caption Usikae karibu na sabuni

"Nikiwa naoga, natengeneza povu la kulilamba lote, na sabuni ikibakia ndogo, naimumunya mdomoni, nasikia raha sana" amesema binti huyo.

"Nahisi nimetakata zaidi. Kula sabuni hunifanya nihisi msafi zaidi" ameongeza mwanadada huyo.

Gazeti la Times of India limesema mbali na kupatiwa matibabu madaktari wameshauri awe anajishughulisha na mambo mengine, na ajitahidi asikae karibu na sehemu zenye sabuni, kama vile bafu..na kadhalika..

Hasira hasara

Bwana mmoja nchini Uchina, alikunywa rangi, baada ya kupoteza fedha zake katika mchezo wa kamari.

Haki miliki ya picha C4
Image caption Rangi

Gazeti la Shanghai Daily limesema Bwana huyo mwenye umri wa miaka arobaini, ambaye hakutajwa jina lake, alikuwa akipenda sana kucheza kamari.

Watu wa lioshuhudia mkasa huo katika wilaya ya Baoshan, wamesema ghafla, alibeba kopo la rangi ya nyumba na kuanza kugida rangi hiyo.

Mara moja alipelekwa katika hospitali iliyo karibu, na madaktari kukadiria kuwa alikunywa takriban nusu kilo ya rangi. Madaktari wamesema huenda wakalazimika kumfanyia upasuaji ili kuitoa rangi hiyo iliyoganda tumboni.

Na kwa taarifa yako.... Pengwini, ni ndege pekee anayeweza kuogelea, lakini hawezi kuruka.

Tukutane wiki ijayo... Panapo majaaliwa

Taarifa kutoka mitandao mbalimbali