Nahodha wa AC Milan Gattuso aomba radhi

Nahodha wa AC Milan Gennaro Gattuso ameomba radhi kwa kumpiga kichwa kocha wa Tottenham Joe Jordan, baada ya timu yake kulazwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza wa timu 16 kuwania ubingwa wa Ulaya.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Gattuso akimkaba koo Joe Jordan

Gattuso anayechezea pia timu ya taifa ya Italia, alizozana na Jordan mwenye umri wa miaka 59 na baadae akamsukuma kichwani.

Nahodha huyo wa AC Milaa mwenye umri wa miaka 33 ambaye siku za nyuma aliwahi kuichezea klabu ya Rangers ya Scotland, anasubiri kuadhibiwa kutokana na vitendo vyake vya utovu wa alivyoonesha uwanjani.

"Nilishindwa kujizuia," alisema Gattuso, ambaye awali alimsukuma Jordan usoni. "Hakuna kisingizo kwa niliyoyafanya. Nabeba lawama zote kwa yote hayo."

Gattuso aliongeza: "Nilikuwa nimekasirika. Sote tulikuwa tukizungumza Kiskochi, lugha ambayo nilijifunza wakati nikicheza katika mji anaotoka kocha huyo wa Glasgow, lakini siwezi kukwambia nini tulichozungumza.

"Sipendelei kuzozana na wachezaji na nimezozana naye, lakini nilikosea kufanya vile nilivyofanya. Nasubiri tu watakachoamua."

Watu hao wawili mapema walikwishazozana kwenye mstari unaogawa uwanja katika kipindi cha pili, baada ya Mathieu Flamini kuoneshwa kadi ya manjano kutokana na rafu mbaya aliyomchezea mlinzi wa kushoto wa Tottenham, Vedran Corluka, huku wengi wakidhani angeoneshwa kadi nyekundu.

Corluka alitolewa kwa machela uwanjani na baadae akaonekana amekaa katika benchi la wachezaji wa akiba akiwa amefungwa plasta gumu na mfuko uliojaa barafu mguuni.

"Meneja wa Tottenham, Harry Redknapp, alisema rafu ya Flamini ilikuwa mbaya sana." "Alipaswa kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Aliingia kwa miguu miwili, ni rafu mbaya sana.

"Ilikuwa rafu ya kuvunja mguu. Corluka atafanyiwa kipimo cha X-ray, lakini sifikirii kama amevunjika, lakini angeweza kuvunjika kwa urahisi."

Rafu aliyocheza Flamini ilibadilisha hali ya mchezo kipindi cha pili kuwa chenye mvutano, huku Gattuso akionekana kuhamaki kila mara.

Awali alizozana na mshambuliaji wa Spurs, Peter Crouch na baadae akaoneshwa kadi ya manjano itakayomfanya asicheze mchezo wa marudiano, baada ya kumchezea rafu Steven Pienaar.

Mwisho wa mchezo, Gattuso alivua fulana yake na haraka akaelekea kumkabili Jordan, akimtolea maneno makali kabla ya kumpiga kichwa.

Gattuso aliondolewa na wachezaji wenzake na akaacha ukali wake na kukumbatiana na mlinzi wa Spurs William Gallas.