Mji wa Libya 'wakumbwa na maandamano'

Image caption Muammar Gaddafi, Rais wa Libya

Mamia ya watu wamepambana na polisi na wale wanaoiunga mkono serikali katika mji wa Benghazi nchini Libya.

Walioshuhudia wameiambia BBC ghasia hizo zilizoibuka usiku zilitokana na kukamatwa kwa mkosoaji mkubwa wa serikali.

Wakili wa mkosoaji huyo baadae alisema kuwa ameachiliwa huru lakini maandamano yakaendelea.

Maandamano ya kuunga mkono demokrasia yameibuka nchi kadhaa za kiarabu katika wiki za hivi karibuni, iliyowalazimisha viongozi wa Tunisa na Misri kuachia madaraka.

Wito umetolewa kwenye mtandao kuwepo kwa maandamano nchini Libya siku ya Alhamis.

'Polisi kujeruhiwa'

Hakuna uthibitisho wa kuwepo maandamano Benghazi, lakini walioshuhudia wanasema katika hatua moja takriban watu 2,000 walihusika.

Walisema polisi walitupiwa mawe ambao inasemekana walijibu mapigo kwa kuwamwagia maji, mabomu ya machozi na risasi za mpira.

Baadae picha ya video ya ghasia hizo iliwekwa kwenye mtandao.

Sehemu ya video hiyo iliwekwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook- ambapo imewekwa na mtu anayedai ilirekodiwa siku ya Jumanne- ilionyesha watu wakishangilia nje ambapo palionekana kama kituo cha polisi.

Milio ya risasi ilikuwa ikisikika, na baadae anaonekana mtu mmoja aliyejeruhiwa akiondoshwa kwenye ghasia hizo.

Televisheni ya taifa ya Libya ilionyesha mamia ya watu huko Benghazi wakiunga mkono serikali.

Mpaka sasa serikali haijatoa kauli yeyote kuhusiana na matukio ya mji huo wa bandari, uliopo takriban kilomita 1,000 mashariki mwa mji mkuu wa Tripoli.

Gazeti la binafsi la Libya kupitia mtandao Quryna limeripoti kuwa, watu 14 walijeruhiwa, wakiwemo maafisa wa polisi 10.