Waziri Habineza wa Rwanda ajiuzulu

Haki miliki ya picha other
Image caption Joseph Habineza

Waziri wa michezo na utamaduni nchini Rwanda Joseph Habineza amejiuzulu.

Hakuna sababu rasmi iliyotolewa kuhusu kujiuzulu kwake lakini hatua hiyo imefanyika siku chache tu baada ya kuhusishwa katika kashfa ya ngono.

Vyombo vya habari nchini humo vilisambaza picha kadhaa alizopigwa akiwa na wasichana kadhaa wakistarehe kwenye nyumba moja mjini Kigali.

Rais Kagame aridhia

Kutoka Kigali mwandishi wetu Yves Bucyana ametuma taarifa ifuatayo.

Taarifa ya kujiuzulu huko kumetolewa na ofisi ya waziri mkuu ambapo ilisemwa kwamba waziri huyo wa utamaduni na michezo Joseph Habineza amejiuzulu na Rais wa Jamuhuri ameridhia hatua hiyo.

Mwandishi wetu wa Kigali Yves Bucyana alisema kwamba Bw Habineza amekuwa akiandamwa na vyombo vya habari kwa kusambaza picha zake za siri alizopigwa akiwa pamoja na wasichana watano.

Waziri huyo pamoja na mabinti hao walikuwa katika hali ya starehe kwenye nyumba moja mjini Kigali.

Kitendo hicho kilitangazwa na vyombo vya habari kama kashfa kwani alikuwa na mabinti hao huku akiwa ni mume wa mtu na pia ikizingatiwa kuwa yeye ni waziri ambaye pia ana majukumu ya kulinda utamaduni wa Wanyarwanda.

Lakini akizungumza na waandishi wa habari Bwana Habineza amepinga namna watu walivyotafsiri picha hizo anazosema ni za zamani.

"Mimi sikuwa na kosa lolote la kujishtaki. Sikuwa na hatia yoyote ila namna watu wanavyozungumzia sakata lenyewe, jinsi wanavyotafsir zile picha na kujaribu kuitia chumvi hiyo wanaoita kashfa. Hiyo ndiyo iliyonifanya kujiuzulu."

Kwa miaka sita aliyotumikia wizara hiyo, pamoja na kuonekana kuwa mtu wa karibu sana na Rais Kagame pia alikuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa na kuwavutia vijana.