Giggs asaini mkataba mpya Man United

Mcheza soka mkongwe Ryan Giggs amesaini mkataba mpya wa mwaka mmoja katika klabu yake ya Manchester United.

Hatua hiyo ina maana mshambuliaji huyo wa pembeni mwenye umri wa miaka 37, atakuwa ameichezea timu hiyo kwa miaka 21 akiwa ameanza kuichezea klabu hiyo tarehe 2 mwezi wa Machi mwaka 1991.

Na akiwa tayari ameshacheza mara 24 msimu huu kwa klabu yake hiyo, Giggs amesema bado anahitaji kutoa mchango zaidi kwa timu yake.

"Ni vizuri kufahamu nachangia mafanikio ya timu. Najihisi bado nahitajika kutoa mchango zaidi," alisema.

"Na hakuna kitu kingine ninachopenda zaidi ya kuichezea United na nimekuwa mwenye bahati sana kufanya hilo kwa miaka 20.

"Huu ni muda wa furaha kuendelea kushirikishwa pamoja na wachezaji wengi hodari vijana ambao wanapitia katika klabu hii."

Giggs ameshaichezea Manchester United zaidi ya mechi 850 na hivi karibuni alicheza mechi yake ya 600 ya Ligi Kuu ya England.