Lampard aonya Chelsea kukumbwa na maafa

Frank Lampard amekiri itakuwa "maafa" iwapo Chelsea itashindwa kufuzu Ligi ya Ubingwa wa Ulaya msimu ujao.

Image caption Frank Lampard

Sare ya kutofungana dhidi ya Fulham siku ya Jumatatu, imewafanya mabingwa hao watetezi kusalia nafasi ya tano ya msimamo Ligi Kuu ya soka ya England.

Chelsea kwa sasa wapo nyuma kwa pointi 12 ya vinara wa ligi hiyo, Manchester United.

Akizungumza katika uzinduzi wa Wakfu wa Wacheza Soka wa England, Lampard ameiambia BBC kitengo cha michezo : "Hatuna budi kumaliza katika timu nne za juu na kamwe hatupaswi kupoteza michezo zaidi, itakuwa "maafa" iwapo hatutafaulu."

Chelsea siku ya Jumamosi itakabiliana na Everton katika mzunguko wa nne wa hekaheka za kuwania Kombe la FA na watapepetana na FC Copenhagen katika mchezo wa kwanza wa mtoano wa Ligi ya Ubingwa wa Ulaya siku tatu baadae.

Na Lampard amekiri mashindano hayo mawili ni muhimu sana kwa klabu yao.

Msambuliaji aliyesajiliwa kwa kitita cha paundi milioni 50 na Chelsea, Fernando Torres ameshindwa kufunga katika mechi mbili alizocheza. Torres alinyakuliwa kwa kitita hicho kutoka Liverpool, lakini Lampard amemtetea nyota huyo wa Hispania katika klabu yake mpya.

Kuhusu mlinzi Luiz aliyesajiliwa kwa paundi milioni 25, Lampard amesema amefurahishwa na usajili walioufanya katika dirisha dogo la usajili mwezi wa Januari, ambapo klabu hiyo imetumia paundi milioni 75.