Watu 104 wauwawa Libya

Shirika la kugombea haki za kibinaadamu, Human Rights Watch, linakisia kuwa watu zaidi ya miamoja wamekufa katika siku chache za fujo za Libya.

Image caption Waandamanaji wanaotaka Gaddafi aachie madaraka

Taarifa kutoka Libya zinaeleza kuwa hali katika mji wa Benghazi ni ya kutisha, siku moja baada ya bunduki za rashasha na silaha kubwakubwa kutumiwa dhidi ya watu waliokuwa kwenye mazishi.

Walioshuhudia matukio ya jana walisema kulikuwa na mtafaruku wakati wanajeshi wa Libya, waliokuwa juu ya mapa, waliwalenga na kuwafyatulia risasi waombolezajii waliokuwa kwenye maziko ya mwandamanaji aliyeuliwa na askari wa usalama.

Daktari mmoja aliiambia BBC kwamba watu wengine waliuwawa mbele ya nyumba zao, na kwamba mahospitali yamejaa maiti.

Maelfu ya raia katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo wamekuwa wakiandamana kuipinga serikali ya nchi hiyo amabayo imekuwa chini ya uongozi wa Kanali Muammar Gaddafi kwa miongo minne sasa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waandamanaji walioko Marekani wakiwaunga mkono raia wa Libya

Kambi ya upinzani imesema shambulio hilo si halali kwani askari hawakuchokozwa lakini kikosi cha usalma kinadai kuwa baadhi ya waandamanaji waliwarushia mabomu.

Libya ni mojawapo ya nchi za kiarabu ambazo zimekumbwa na maandamano baada ya raia wa nchi za Tunisia na Misri kuandamana na kuwalazimisha marais wa nchi hizo kujiuzulu.

Rais wa Tunisia Zine El Abidine Ben Ali aliikimbia nchi yake Januari mwaka huu naye rais Hosni Mubarak wa Misri alijiuzulu Februari 11.