Rais Museveni anukia awamu nyingine kama rais

rais Museveni Haki miliki ya picha AFP
Image caption rais Museveni

Matokeo ya uchaguzi wa urais yanaendelea kutolewa nchini Uganda, huku mgombea wa chama tawala, rais Yoweri Museveni, akielekea kushinda awamu nyingine kama rais wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi nchini humo, Bardu Kiggundu, rais Museveni ambaye ametawala taifa hilo kwa miaka 25, amepata asilimia 67.99 ya kura milioi 7.7 zilizohesabiwa.

Idadi hiyo ni asilimia 55 ya kura zote zilizopigwa. Kufikia sasa matokeo kutoka asilimia 92 ya vituo vya kupigia kura yametolewa rasmi.

Mpinzani mkuu wa rais Museveni, Dr. Kizza Besigye, ambaye amelalamika kuwa uchaguzi huo umekumbwa na dosari nyingi amepata asilimia 26.28.

Ripoti zinasema kuwa mawaziri kadhaa wa serikali wamepoteza viti vyao vya ubunge kwa wagombeaji wa vyama vya upinzani.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kizza Besigye

Tume ya uchaguzi nchini humo inatarajiwa kutangaza matokeo rasmi kabla ya saa kumi na moja jioni saa za Afrika Mashariki.

Wachunguzi kutoka Jumuiya ya Madola na Muungano wa Ulaya wanatarajiwa kutoa ripoti yao kuhusu uchaguzi huo baadaye hii leo.

Kutokana na matokeo hayo , Rais Museveni anaelekea kushinda awamu nyingine kama rais wa Uganda, na kujumuika na marais Robert Mugabe wa Zimbabwe na Muammar Gaddaffi wa Libya kama miongoni mwa marais waliotawala kwa zaidi ya miaka 30.