Chelsea yaizaba Copenhagen 2-0

Chelsea imezinduka baada ya kutolewa katika kombe la FA na kuizaba FC Copenhagen kwa mabao 2-0 katika michuano ya klabu bingwa Ulaya.

Image caption Anelka na Drogba, ambaye alianzia benchi

Mabao yote mawili ya Chelsea yamefungwa na Nicolas Anelka katika dakika za 17 na 54.

FC Copenhagen wakicheza nyumbani hawakuonesha cheche zozote, na kuifanya Chelsea kucheza kwa uhuru katika mchezo wa kwanza wa timu 16 bora.

Mshambuliaji mpya wa Chelsea Fernando Torres licha ya kuanza, bado hajaweza kupata bao lake la kwanza kwa timu hiyo. Drogba alianzia benchi.

Katika mchezo mwingine Real Madrid ililazimishwa sare na FC Lyon ya Ufaransa kwa kutoka sare ya 1-1.

Image caption Karim Benzema

Karim Benzema, alifunga bao hilo la Real, muda mfupi baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba baada ya Emmanuel Adebayor kutoka katika dakika ya 65.

Bafetimbi Gomis wa Lyon alisawazisha bao hilo katika dakika ya 85.