Watano Man United kutocheza na Marseille

Manchester United katika pambano lao dhidi ya Marseille la Ligi ya Ubingwa wa Ulaya, itawakosa wachezaji wake watano ambao ni majeruhi. Wachezaji hao ni Anderson, Rio Ferdinand, Ryan Giggs, Jonny Evans na Michael Owen.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Wachezaji wa Manchester United

Ni Anderson pekee aliyecheza siku ya Jumamosi katika mchezo wa Kombe la FA walipoilaza Crawley Town na kiungo huyo Mbrazil alitolewa nje wakati wa mapumziko.

Nahodha Ferdinand hajacheza tangu alipoumia goti kabla ya kupambana na Wolves tarehe 5 mwezi huu wa Februari, wakati beki mwenzake wa kati Evans ana matatizo ya kifundo cha mguu.

Giggs na Owen walicheza dhidi ya Manchester City tarehe 12 mwezi huu wa Februari.

Lakini mshambuliaji Owen inasemekana ana matatizo ya nyonga.

Kuendelea kwa matatizo ya majeruhi katika safu ya ulinzi ya Manchester United ina maana Chris Smalling huenda akaanza pamoja na Nemanja Vidic kwa pambano hilo la Marseille siku ya Jumatano katika uwanja wa Stade Velodrome.

Meneja wa United Sir Alex Ferguson, amewajumuisha katika kikosi chake walinzi mapacha wa Brazil Rafael and Fabio, licha ya machezaji hao kutoka nje baada ya kuumia walipoilaza Crawley 1-0 katika uwanja wa Old Trafford.

Chipukizi wawili Joshua King na Ryan Tunnicliffe pia wamejumuishwa katika kikosi hicho pamoja na Gabriel Obertan na Bebe.

Marseille ilifuzu kuingia hatua ya mtoano katika kundi F nyuma ya Chelsea, lakini nao watamkosa mshambuliaji wao hatari Andre-Pierre Gignac, aliyejeruhiwa wiki iliyopita.