Fifa yatoa salamu za rambirambi Somalia

Rais wa Fifa Sepp Blatter ametoa salamu za rambirambi kwa Somalia baada ya mcheza soka hodari chipukizi kuuawa kutokana na shambulio la bomu la kujitoa muhanga lililotokea mjini Mogadishu.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Hospitali ya Dagaal ikipokea majeruhi

Mchezaji huyo anayechezea timu ya taifa ya Somalia chini ya umri wa miaka 20, Abdi Salaan Mohamed Ali, ni miongoni mwa watu wa 10 waliouawa baada ya gari lililosheheni mabomu kulipuka siku ya Jumatatu.

Wachezaji wengine wawili, Mahmoud Amin Mohamed na Siid Ali Mohamed Xiis, ni miongoni mwa wachezaji 35 waliojeruhiwa katika shambulio hilo.

Blatter amemwandikia barua ya mkono wa pole Rais wa Shirikisho la Soka la Somalia Said Mahmoud Nur, akisema "kwa huzuni kubwa, tumepokea taarifa za tukio hilo".

"Kwa niaba ya Fifa... Napenda kutoa salamu za rambirambi kwako, wapenda soka wa Somalia na zaidi familia, marafiki na wote waliowapenda marehemu," ilisema taarifa hiyo ya Sepp Blatter.

Ali alikufa baada ya kupigwa na mlipuko huo alipokuwa mazoezini katika uwanja karibu na chuo cha polisi ambacho kililengwa na mshambuliaji wa kujitoa muhanga, wakati Mohamed na Xiis walijeruhiwa walipokuwa wakirejea nyumbani.

Kundi la wapiganaji wa Kiislamu lilidai kuhusika na shambulio hilo.