UN yalaani vurugu dhidi ya raia Libya

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Kanali Gaddafi.

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limeshutumu vikali matumizi ya nguvu dhidi ya raia nchini libya, na kutoa wito kwa wale wanaohusika katika uovu huo dhidi ya raia kuwajibikia makosa yao.

Taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo ya dharura mjini New York imetaka kukomeshwa vurugu mara moja na kutoa wito kwa maafisa kushugulikia malalamishi ya wananchi wa Libya.

Lakini baraza hilo halikushughulikia ombi la naibu balozi wa Libya katika umoja wa mataifa, Ibrahim Dabbash, la kutaka anga zote za Libya kufungwa ili kuzuia mashambulio dhidi ya waandamanaji.

Bwana Dabbash amesema wanajeshi wa serikali wameanza kuwashambulia raia magharibi mwa Libya.

Awali waziri wa usalama wa ndani wa Libya, Abdel Fatah Yunes, alijiunga na orodha inayozidi kukuwa ya maafisa wa ngazi ya juu katika serikali ya bwana Gaddafi wanaojiuzulu. Ametaka jeshi la taifa hilo kujiunga katika mapinduzi ya kumng'oa madarakani kanali Gaddafi.

Spika wa bunge la Libya alitoa tangazo kwenye televisheni ya kitaifa kuhusu kile alichokitaja kuwa uchunguzi ulio huru kuhusu matukio ya hivi punde.

Kadhalika amesema serikali inabuni msururu wa sheria mpya, ikiwemo sheria za vyombo vya habari na katiba ya kudumu.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maandamano mashariki ya kati.

Hapo awali katika hotuba yake kubwa zaidi tangu maandamano kuanza wiki iliyopita, Kanali Muammar Gaddafi alisema kuwa yuko tayari kufa nchini mwake iwapo italazimika. Akizungumza nje ya mahali aliposema kuwa ni makao yake mjini Tripoli, Gaddafi alitoa wito kwa wafuasi wake kujitokeza mitaani kuvunja maandamano dhidi ya serikali.

Bw Gaddafi alisema kutokana na utawala wake, Libya imekuwa taifa linaloongoza duniani.

''Mimi ni mpiganaji, mimi ni mpiganaji kutoka vijijini, kutoka jangwani. Nimepigana mijini na vijijini katika mapinduzi ya kihistoria yaliyoleta heshima kwa nchi ya Libya. Watajivunia mafanikio yake kizazi baada ya kizazi,'' akasema kanali Gaddaffi.

''Babu yangu Abdulsalam Bu-Munyar ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kujitoa mhanga wakati wa vita. Kwa hivyo siwezi nikavunja.Sitaondoka kwenye ardhi hii ya nchi yangu yenye heshima. Nitajitolea mhanga kupigania nchi yangu hadi mwisho!'' akafoka tena.

Gaddafi alionya kuwa mtu yeyote atakayeshiriki katika maandamano hayo kuwa atahukumiwa kifo.

Aidha aliwaaita waandamanaji kuwa ni mende au panya.

Kufuatia hotuba hiyo, katika eneo la Green Square raia wengi wanahofia kuwa hali huenda ikawa mbaya zaidi.

Zaidi ya watu mia tatu wameuwawa tangu maandamano hayo yaanze.