Ancelotti apongeza washambuliaji Chelsea

Meneja wa Chelsea, Carlo Ancelotti amewapongeza washambuliaji wa timu yake baada ya kuwalaza FC Copenhagen 2-0 katika mchezo wao wa awali wa hatua ya mtoano kwa timu 16 zinazowania Ubingwa wa Ligi ya vilabu vya Ulaya.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Carlo Ancelotti

Nicolas Anelka alifunga mara mbili baada ya kuanza kucheza pamoja na Fernando Torres, wakati Didier Drogba na Salomon Kalou waliingia baadae.

Alipoulizwa iwapo wao ni bora barani Ulaya, Ancelotti alisema: "Ndiyo, Nahisi hivyo.

"Tunachohitaji ni kuweza kuwa na washambuliaji hawa katika hali nzuri, lakini kuwabadilisha kunaweza kuwafanya wawe imara zaidi hasa katika michezo ya Ligi Kuu ya soka ya England."

Ushindi huo ilikuwa ni faraja kubwa kwa Ancelotti, ambaye timu yake iliondolewa katika mashindano ya Kombe la FA na Everton siku ya Jumamosi, huku wakijitahidi kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu ya England.