Obama alaani ghasia nchini Libya

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Eneo la Benghazi nchini Libya

Rais Barrack Obama wa Marekani amelaani machafuko yanayo endelea nchini Libya, katika hotuba yake ya kwanza kwenye runinga tangu mageuzi yaanze nchini Libya, yapata wiki moja sasa. Amesema kuwa ukatili unaotumiwa na vyombo vya serikali kukabili waandamanaji haukubaliki kamwe na kuwa serikali yake inatathhmini hatua za kuchukua.

Japo hakutoa maelezo zaidi, alidokeza kuwa waziri wa mashauriano ya nje Hillary Clinton atasafiri mjini Geneva, Uswizi, kushauriana na nchi zingine.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais Obama akizungumza kuihusu Libya

Huku hayo yakiarifiwa maelfu ya waandamanaji wanaopinga serikali wamekuwa wakisherehekea kile wanachokiita ushindi mkubwa Mashariki mwa Libya.

Wakaazi mjini Tripoli wamesema wanaogopa kutoka nje kwa sababu wana wasiwasi wanajeshi wanaounga mkono serikali huenda wakawafyatulia risasi.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema yamethibitisha kuwa watu wasiopungua mia tatu wameuwawa tangu makabiliano hayo kuanza wiki iliyopita.