Raouraoua ateuliwa Kamati Kuu ya Fifa

Rais wa Shirikisho la Soka la Algeria, Mohamed Raouraoua, amechaguliwa kuingia katika Kamati ya Utendaji ya Fifa.

Raouraoua amechukuwa nafasi moja kati ya mbili, huku Mkuu wa Shirikisho la Soka la Ivory Coast, Jacques Anouma ameendelea kushikilia nafasi yake.

Raouraoua amechukua nafasi ya Amos Adamu wa Nigeria, ambaye amesimamishwa na Fifa kwa tuhuma za kuomba rushwa wakati wa hekaheka za kutafuta nchi zitakazoandaa mashindano ya Kombe la Dunia kwa mwaka 2018 na 2022.

Mtu aliyehusika na maandalizi ya ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini, Danny Jordaan alitupwa nje kwa kupata kura 10 tu na kushika nafasi ya pili nne.

Raouraoua alishinda kura 39, wakati Anouma alichaguliwa kwa kipindi cha pili cha miaka minne kwa kuzoa kura 35 katika uchaguzi uliofanyika nchini Sudan.

Suketu Patel wa Ushelisheli alikusanya kura 12 baada ya kumwangusha Jordaan, wakati mwenzake Adam kutoka nchi moja Nigeria, Ibrahim Galadima, alimaliza wa mwisho kwa kura tano tu.

Wajumbe wote wa nchi 53 wa Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) wana kura mbili.

Kalusha Bwalya wa Zambia alijitoa mapema mwezi huu, lakini mchezaji huyo bora wa Afrika wa mwaka 1988, bado anayo mengi ya kushangilia akiwa Khartoum.

Rais wa Chama cha Soka cha Ghana, Kwesi Nyantakyi pia alishinda katika uchaguzi huo wa Jumatano, ambapo alizoa kura 34 na kumshinda Anjorin Moucharafou wa Benin katika eneo la Magharibi B.

Naye nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Leodegar Tenga ambaye ni Rais wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo, ameshinda kwa kumbwaga mpinzani wake kutoka Rwanda, Celestin Musabyimana na kupata ujumbe wa Kamati ya Utendaji kwa eneo la Kati na Mashariki mwa Afrika.

Kwengineko, Tarek Bouchamaoui wa Tunisia kwa eneo la Kaskazini, Omari Constant wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo eneo la Kati na Almamy Kabele Camara wa Guinea akiwakilisha eneo la Magharibi A, wote walichaguliwa bila kupingwa.