Maandamano zaidi Tunisia

Polisi wamewatawanya waandamanaji katika mji mkuu wa Tunis siku ya Ijumaa wakidai kujiuzulu kwa Mohammed Ghannouchi, ambaye amekuwa akiongoza nchi hiyo baada ya Ben Ali kuikimbia Tunisia mapema mwaka huu.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Waandamanaji nchini Tunisia

Ulikuwa umati mkubwa zaidi tangu Rais Ben Ali kuikimbilia Saudi Arabia mwezi uliopita.

Ben Ali alikuwa Rais wa Tunisia kwa kipindi cha miaka 23 na alitimuliwa baada ya wiki kadhaa za maandamano.

Bw Ghannouchi na serikali yake ya mpito walitangaza wataanda uchaguzi utaofanyika mwezi wa Julai.

Lakini waandamanaji wanaonekana kutoridhishwa na walikuwa wakiimba mitaani 'Ghannouchi ondoka.'

Polisi walifyatua risasi za ilani na mabomu ya kutoa machozi karibu na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Walioshuduia tukio hilo wanasema mtu mmoja tu ndiye aliyejeruhiwa miongoni mwa waandamanaji takriban 100,000.

Bw Ghannouchi aliwahi kufanya kazi katika serikali ya Ben Ali tangu mwaka 1999.