Birmingham mabingwa Carling

Birmingham City imeshangaza wengi kwa kuichapa Arsenal 2-1 katika fainali ya Kombe la Carling.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Obafemi Martins baada ya kupachika bao la ushindi

Arsenal, waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya ushindi katika mchezo huo kwenye uwanja wa Wembley, walishindwa kutumia fainali hii kumaliza ukame wa vikombe katika klabu hiyo.

Nicola Zigic wa Birmingham aliandika bao la kwanza katika dakika ya 28, kufuatia mpira wa kona kupigwa.

Image caption Arsene Wenger

Nahodha wa Arsenal katika mchezo huo Robin Van Persie akiongoza kwa mifano, alisawazisha bao hilo dakika sita kabla ya mapumziko.

Arsenal waliendelea kulisakama lango la City, lakini kipa Ben Foster alisimama imara hasa kwa kuzuia mikwaju ya Samir Nasri na Niklas Bendtner.

Mambo yalibadilika wakati mashabiki wakidhani huenda mchezo ukaenda katika dakika za nyongeza.

Image caption Alex McLeish, kocha wa City

Bao la ushindi la City lilipatikana katika dakika ya 89 baada ya kipa wa Arsenal Wojsiech Szczesny na beki wake Laurent Koscielny kujichanganya na kumpa nafasi Obafemi Martins kufunga bao aliloliita jepesi zaidi maishani mwake.

Ushindi huu unaipa nafasi City kucheza Ulaya msimu ujao. Mara ya mwisho Birmingham kushinda ushindi kama huu ilikuwa mwaka 1963.

Mara ya mwisho kwa Arsenal kunyakua kombe muhimu, ilikuwa mwaka 2005.