West Ham yaivuta mkia Liverpool 3-1

Nahodha Scott Parker ameihamasisha West Ham kuitandika Liverpool kwenye mechi iliyopigwa Upton Park, matokeo ambayo yameinyanyua kutoka mkiani mpaka nafasi ya 18 katika msimamo wa Ligi kuu ya soka ya England.

Parker alidokoa mpira ulioingia pembeni mwa mlinda mlango Pepe Reina katika dakika ya 22 kuipatia West Ham goli la kuongoza.

Kisha Demba Ba akapiga mpira wa kichwa kuandika goli la pili katika mechi ambayo Liverpool walionekana kuduwazwa.

Hata hivyo dakika za mwisho Liverpool waliongeza jitihada ndipo Glen Johnson alipofunga goli la kufutia machozi katika dakika ya 84.

Hadithi haikushia hapo, Carlton Cole alihakikisha ushindi mnono pale alitumbukiza mpira na kufanya idadi ya magoli kuwa 3-1.

Katika mchezo mwingine Manchester City imetoka sare ya 1-1 na Fulham. Bao la City lilifungwa na Mario Balotelli, huku goli la Fulham likifungwa na Damian Duff.