Ubingwa wa Afrika Zamalek yasonga mbele

Zamalek imeingia ngwe ya pili ya kuwania ubingwa wa vilabu barani Afrika, baada ya kuilaza Ulinzi Stars ya Kenya 1-0 mjini Cairo.

Image caption Kombe la Caf

Wamisri walioshinda pambano hilo kwa bao la kipindi cha pili lililofungwa na Mahmud Abdel Razek.

Zamalek wamefanikiwa kuingia ngwe ya pili ya mashindano hayo baada ya ushindi wa jumla ya mabao 5-0.

Mpambano huo ulikuwa ufanyike wiki mbili zilizopita, lakini uliahirishwa kutokana na na ghasia za kimapinduzi zilizomuondoa madarakani Rais Hosni Mubarak.

Serikali mjini Cairo iliruhusu mashabiki kuhudhuria mechi hiyo, katika uwanja wa jeshi.

Hiyo ilikuwa ni mechi ya kwanza rasmi kuchezwa mjini Cairo tangu mapinduzi hayo yalipotokea.

Wachezaji wa timu zote mbili walifunga vitambaa vyeusi, kuwakumbuka watu waliopoteza maisha katika vuguvugu hilo maarufu.

Wakati huo huo, Wydad Casablanca ya Morocco pia ilifanikiwa kusonga mbele ngwe ya pili licha ya kufungwa 1-0 na Aduana Stars ya Ghana.

Aduana Stars walikuwa na matumaini ya kulipa deni la kufungwa mabao 3-0 katika mchezo wa awali, wakati Bernard Dong Bortey alipoifungia timu hiyo kwa mkwaju wa penalti dakika ya 37 na kurejesha matumaini ya kushinda mchezo huo.

Katika michezo mingine mwishoni mwa wiki, AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, iliilaza Ocean View ya Zanzibar3-0 na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-1; JCA Treichville ya Ivory Coast iliilaza AS FAN ya Niger 3-0 na kusonga mbele na ASEC Mimosas, pia ya Ivory Coast iliichabanga ASC SNIM kutoka Mauritania 2-0 na kufanikiwa kusonga mbele raundi ijayo kwa jumla ya mabao 9-0.