Ubakaji Congo 'wawanyima watoto elimu'

Image caption Wanawake wakipinga ubakaji Congo

Mfuko wa elimu wa umoja wa mataifa Unesco umesema vita vinawakosesha watoto milioni 28 duniani kupata elimu kutokana na kudhalilishwa kijinsia na kushambuliwa wakiwa shuleni.

Mwandishi wa ripoti hiyo aliiambia BBC eneo lililoathirika zaidi ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akiita "mji mkuu wa ubakaji duniani."

Unesco ilisema, theluthi ya matukio ya ubakaji yanayoripotiwa Congo huhusisha watoto.

Taarifa hiyo pia imesema kufikia malengo ya elimu kwa wote ya umoja wa mataifa ifikapo mwaka 2015, Afrika inahitaji takriban walimu wapya milioni mbili.

Kevin Watkins, mwandishi wa ripoti hiyo 'The hidden crisis' aliiambia BBC, "Huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huenda takriban nusu ya watoto waliofikia umri wa kuanza shule ya msingi hawapo shuleni."

Alisema mahudhurio ya watoto wa kike nchini Congo ni machache ukilinganisha na maeneo mengine kusini mwa jangwa la Sahara.

" Sababu mojawapo ni kutokana na eneo hilo kuwa kiini cha ubakaji duniani ambapo imeleta athari kubwa katika mfumo wa elimu."

Alisema, udhalilishaji wa kijinsia unaathiri uwezo wa kujifunza na kusababisha woga unaomfanya mtoto wa kike kubaki nyumbani.

Jeshi dhidi ya bajeti za elimu

Alisema, wanamgambo hulenga mamlaka muhimu wanaposhambulia vijiji, ikimaanisha shule na zahanati ndio mara nyingi hubomolewa.

Ripoti ya Unesco nayo imeelezea kwa kirefu namna mashambulio shuleni nchini Afghanistan ilivyoongezeka kwa asilimia 77, kutoka 347 mwaka 2008 hadi 613 mwaka 2009.

Na pia inasema kaskazini mwa Yemen shule 220 zimebomolewa, au kuharibiwa wakati wa mapigano yaliyotokea miaka miwili iliyopita.

Inatoa wito kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita kuchukua hatua thabit zaidi katika kuwashtaki wanaohusika na udhalilishaji kijinsia na kutaka kuundwe kwa tume ya kimataifa.

Uwekezaji mdogo katika elimu nao umetajwa.

Ripoti hiyo imetaja nchi 21 maskini duniani ambazo hutumia fedha nyingi kwenye bajeti ya kijeshi kuliko elimu ya msingi.

Kwa mfano, Chad, hutumia mara nne ya bajeti yake kwenye silaha kuliko shule za msingi.

Hata hivyo ripoti hiyo imeelezea mafanikio ya kuongeza idadi ya waliojiandikisha mashuleni barani Afrika.