Maafisa wa UM washambuliwa Ivory Coast

Umoja wa Mataifa umesema maafisa wake walishambuliwa nchini Ivory Coast walipokuwa wakipeleleza taarifa za ukiukaji wa sheria za vikwazo vya silaha vilivyowekewa nchi hiyo.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kikosi cha Umoja wa Mataifa likishika doria nchini Ivory Coast

Maafisa hao walishambuliwa wakiwa katika mji mkuu wa Yamoussoukro.

Walikuwa wakichunguza ripoti kwamba Belarus ilitoa helikopta kuwafadhili wafuasi wa Laurent Gbagbo ambaye amekataa kuachia madaraka.

Umoja huo umesema haujafanikiwa kuthibitisha taarifa kuhusu shehena hiyo lakini maafisa wake wataendelea kufuatilia hali nchini humo.

Mkutano ulioandaliwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili ripoti hiyo imefutwa.

Wakati huo huo, waasi wa zamani wa Ivory Coast walisema wako tayari kujihami na kupambana dhidi ya Bw Gbagbo.

Msemaji wa kundi hilo la New Forces, Cisee Sindou, aliiambia BBC kwamba iwapo mtafaruku utaendelea baina ya wafuasi wa Bw Gbagbo na hasimu wake Alassane Ouattara, kundi hilo litachukua hatua.

Lakini Bw Sindoue alisema kuwa hakuna operesheni ya kivita iliyopangwa.

Bw Ouattara anatambuliwa na wengi kama mshindi wa uchaguzi wa urais wa Novemba mwaka jana.

Bw Gbagbo na Bw Ouattara hawajatoa kauli yoyote kuhusiana na ilani aliyotoa msemaji huo wa waasi.