'Ubaguzi' waigawanya Afrika Kusini

Image caption Trevor Manuel

Mmoja wa mawaziri wenye ushawishi mkubwa, Trevor Manuel, amemtuhumu msemaji wa serikali kwa "mfumo mbaya zaidi wa ubaguzi" kutokana na kauli alizotoa kuhusu machotara.

Bw Manuel alitoa kauli hizo katika barua iliyochapishwa katika gazeti moja nchini humo.

Msemaji huo Jimmy Manyi alisema katika mahojiano mwaka jana- iliyoibuka hivi karibuni- kwamba kuna " machotara wengi sana" katika jimbo la Western Cape.

Bw Manyi hajasema lolote mpaka sasa.

Bw Manuel, waziri anayeshughulikia sera za kiuchumi kwenye ofisi ya Rais, ni waziri wa kwanza kuzungumzia suala hilo.

Bw Manuel ni kiongozi mwandamizi wa jumuiya ya machotara katika serikali ya Afrika Kusini.

"Sasa ninatambua Nelson Mandela alikuwa akimzungumzia nani aliposema akiwa kizimbani kuwa alipambana dhidi ya ukandamizaji wa watu weupe na pia alipambana dhidi ya ukandamizaji wa watu weusi- Jimmy, alikuwa akizungumzia kupambana na watu kama wewe."

Bw Manyi alitoa kauli hizo katika mahojiano ya televisheni Machi 2010, alipokuwa mkurugenzi wa idara ya kazi.

Chama tawala cha Africa National Congress (ANC) tangu wakati huo haijajihusisha na kauli za Bw Manyi, kikisema kauli hizo zilikuwa "zinasumbua" na "hazikubaliki".

Idara ya habari ya serikali imeomba radhi kwa niaba ya Bw Manyi.