Ferguson amjia juu mwamuzi Atkinson

Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amesema "alihofu mambo yangekuwa mabaya", baada ya Martin Atkinson kuchaguliwa kuchezesha mtanange wao dhidi ya Chelsea ambapo walifungwa 2-1 Chelsea.

Image caption Sir Alex Ferguson

Manchester United walipoteza mchezo huo baada ya kufungwa bao la mkwaju wa penalti na Frank Lampard, iliyoonekana na utata katika dakika ya 80, baada ya Yuri Zhirkov kuangushwa chini na mlinzi Chris Smalling.

"Unahitaji kuwa na mwamuzi atakayechezesha kwa haki-mwenye msimamo usiyoyumba-na hakutukupata hayo," alisema Ferguson.

"Wakati nilipoona nani atachezesha, niliingiwa na hofu. Nilitarajia mambo hayatakuwa mazuri."

Ferguson pia alikasirika baada ya mlinzi wa Chelsea David Luiz, kutooneshwa kadi ya pili ya manjano baada ya kumtengea na kumuangusha mshambuliaji wake Wayne Rooney katika eneo karibu na sanduku la hatari la lango la Chelsea.

Badala yake, Atkinson akaashiria mchezo uendelee, wakati Chelsea wakiwa wametapakaa uwanjani, kabla mwamuzi kuipatia adhabu ya penalti Chelsea baada ya Zhirkov aliyeingia kipindi cha pili kuanguka chini kutokana na kuzuiwa na Smalling.

"Ni jambo la kushangaza. Hata kabla ya tukio hilo, Luiz alimfanyia rafu mbaya Chicharito akiwa hana mpira," alisema Ferguson.

"Uamuzi wake ulibadilisha kabisa matokeo ya mchezo. Na ataendelea kuchezesha kila wiki."

Atkinson msimu uliopita alishutumiwa na Ferguson timu hizo mbili zilipopambana katika uwanja wa Stamford Bridge, baada ya kutoa adhabu ya mwakju wa free kick, ambapo Ferguson anaamini haikupaswa kutolewa, ambapo John Terry alifunga bao moja la ushindi.