Magazeti yasitishwa Ivory Coast

Magazeti ya Ivory Coast yamesitisha uchapishaji wakipinga kile wanachosema ni unyanyasaji kutoka kwa wafuasi wa Rais Laurent Gbagbo.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Laurent Gbagbo

Magazeti hayo, ambayo siyo ya kiserikali na baadhi yake humuunga mkono Alassane Ouattara, yamedai kuwa kwa miezi miwili sasa wamekuwa wakinyanyaswa.

Bw Gbabgo amekataa kuachia madaraka na hii ni baada ya uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi Novemba mwaka jana.

Bw Ouattara anatambuliwa na wengi kuwa ndiye aliyeshinda uchaguzi huo.

Vurugu kati ya wafuasi wa Ouattara na Gbabgo imesababisha Umoja wa Mataifa kutoa onyo kwamba nchi hiyo inakaribia kuingia katika hali ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Uasi wa mwaka 2002 uliigawanya nchi hiyo katika pande mbili; kaskazini ikidhibitiwa na kundi la New forces na kusini ikiwa chini ya serikali.

Wamiliki wa magazeti hayo tisa inayojumuisha Le Nouveau Reveil, Le Patrote na Nord Suf wamesema kuwa wamesitisha uchapishaji wa magazeeti hayo kwa muda usiojulikana.

Akizungumza na AFP msemaji wa magazeti hayo Dembele Al Seni alisema 'waandishi wetu wa habari wako katika hatari ya kuuawa kila wakati.'

Magazeti hayo pia yalisema huwa wanatozwa faini kila mara na chombo cha urekebishaji wa vyombo vya habari cha Ivory Coast.

Bw Gbagbo hajatoa kauli yoyte kuhusu madai hayo.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za waandishi wa habari, Reporters Without Borders, limesema wasiwasi wao kuhusu uhuru wa waandishi wa habari nchini humo unaendelea kupanda.

'Tutatoa usaidizi wetu kwa magazeti hayo yasiyo ya kiserikali yanayotishiwa na tumeamua kuilaani hali hii ambayo imekuwa mbaya zaidi kwa waandishi wa habari nchini humo' shirika hilo lilisema.

Shirika hilo pia limelaani tukio ambapo mwandishi wa habari aliuawa kwa kuvamiwa na umati wa watu.

Mwanahabari huyo alikuwa mwajiriwa wa gazeti linalomuunga mkono Gbagbo huko mjini Abidjan ambapo wafuasi wengi wa Ouattara huishi.

Liliongeza pia kuwa kituo cha kurusha matangazo cha RTI iliyomilikiwa na serikali na kudhibitiwa na wafuasi wa Gbagbo kilishambuliwa na wafuasi wa Ouattara mjini Abidjan hivi karibuni.