Anga ya Libya huenda ipigwe marufuku

Waasi wa Libya Haki miliki ya picha bbc

Shirika la kujihami barani Ulaya,NATO pamoja na Washirika wake na Jumuiya ya nchi za Kiarabu zinatafakari hatua za kuthibiti wanajeshi watiifu kwa Kanali Muammar Gaddafi dhidi ya kuendelea kuwashambulia raia.

Kuna mazungumzo ya kupiga marufuku ndege kupaa anga ya Libya kama njia ya kulinda raia na kuwapa nguvu zaidi waasi. Hata hivyo pendekezo hili linaonekana kukumbwa na hatari kadhaa.

Wanadiplomasia kutoka Jumuiya ya Ulaya na Muungano wa Afrika wameunga mkono hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi ya utawala wa Libya.

Hali hii ilipelekea baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kutangaza vikwazo dhidi ya Kanali Gaddafi na washirika wake wiki jana.Tangu hapo Jumuiya ya nchi za kiarabu zimekua zikitafakari kutangaza marufuku ya ndege kupaa anga ya Libya.

Aidha pendekezo hilo linaungwa mkono na Muungano wa Afrika hasa ikiwa mashambulio dhidi ya raia yakiendelea.Hata hivyo AU imepinga mpango wowote wa kijeshi kutoka nchi za magharibi.