Arsenal yabanwa, West Hama yacharuka

West Ham imefanikiwa kupata ushindi wa pili mfululizo wakicheza nyumbani kwao baada ya kuwalaza Stoke 3-0 na kujinaqsua kutoka mkiani.

Haki miliki ya picha pa
Image caption West Ham wakishangilia bao

Kujichanganya kwa walinzi wa Stoke kulimfanya Demba Ba kufunga bao la kuongoza, huku Manuel da Costa akiongeza bao la pili kwa kichwa kabla ya mapumziko.

Stoke walicharuka baada ya kuingizwa Matthew Etherington na Kenwyne Jones, lakini hawakuweza kufua dafu mbele ya walinzi wa West Ham.

Bao la tatu la West Ham liliwekwa wavuni na Hitzlsperger baada ya walinzi wa Stoke kushindwa kuondoa hatari langoni baada ya Piquionne kufumua mkwaju.

Stoke walijitahidi kutafuta bao la kufutia machozi, lakini ngiome ya West Ham ilikaa imara na kuwawezesha wenyeji kupata ushindi wa pili mfululizo wa Ligi nyumbani, kwa mara ya kwanza tangu mwezi wa Aprili mwaka jana.

Matokeo hayo yameiwezesha West Ham kupata pointi 31 wakiwa sasa katika nafasi ya 17, wanazichungulia Birmingham, Wolves na Wigan wanaoshikilia mkia.

Arsenal wameshindwa kutumia vizuri nafasi ya kupunguza wigo wa pointi na vinara wa Ligi Kuu ya England Manchester United kwa pointi moja, baada ya kubanwa na Sunderland kwa kutoka sare ya kutofungana kwenye uwanja wa Emirates.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Nicolas Bentner

The Gunners walikuwa wanafahamu fika kwamba Manchester wakijiandaa kucheza ugenini na Liverpool siku ya Jumapili, walikuwa na nafasi nzuri ya kujisogeza kileleni tangu msimu wa mwaka 2004.

Lakini jitahada zao hadi wakati wa mapumziko ziliishia ukingoni, huku Samir Nasri na Marouane Chamakh wakikosa nafasi nzuri za kufunga, kwa mikwaju yao ikigonga mwamba wa lango na Andrey Arshavin alishindwa kufunga mkwaju wake alipouelekeza pembeni.

Sunderland, ambao walipoteza mechi zao nne zilizopita, walicheza vizuri kipindi cha kwanza na nusura wangefunga bao katika kipindi cha pili dakika za mwisho za kipindi cha pili baada ya Danny Welbeck kupoteza nafasi nzuri kwa mkwaju uliopanguliwa na mlinda mlango wa Arsenal.

Matokeo hayo bado yameibakisha Arsenal nafasi ya pili wakiwa na pointi 57, huku Sunderland wakijikusanyia pointi 38 katika nafasi ya nane.

Bolton wamefanikiwa kupata pointi tatu nyumbani na kuweza kushika nafasi ya sita na kuwaporomosha kwa nafasi moja Liverpool, baada ya kuwalaza Aston Villa 3-2 kwa bao la ushindi likifungwa na Ivan Klasnic dakika ya mwisho.

Haki miliki ya picha pa
Image caption Pambano Bolton na Aston Villa

Darren Bent alipoteza nafasi nzuri ya kufunga baada ya kupata nafasi nzuri ya kubakia na mchezji mmoja wa Biolton, lakini akajirudi na kupachika bao la kwanza kwa mkwaju wa karibu.

Gary Cahill akaisawazishia Bolton kwa kichwa dakika chache kabla ya mapumziko, lakini Marc Albrighton akaifungia Villa bao la pili.

Jussi Jaaskelainen aliokoa mkwaju wa penalti wa Ashley Young kabla ya Cahill kuisawazishia tena Bolton kwa mkwaju wa mguu wa kushoto na Klasnic aliyeingia kipindi cha pili, akaipatia ushindi huo muhimu Bolton kwa mkwaju wa yadi 14.

Na mkwaju wa adhabu ya penalti dakika za mwisho ulioonekana na utata, uliipatia Fulham ushindi wa 3-2 dhidi ya Blackburn katika mpambano mkali uwanja wa Craven Cottage.

Haki miliki ya picha pa
Image caption Fulham wakishangili ushindi

Damien Duff alitangulia kuipatia bao Fulham, lakini Rovers wakasawazisha kwa bao la Grant Hanley.

Duff kwa mara nyingine alifungia Fulham bao la pili, kabla ya mkwaju wa juu wa David Hoilett ulioipatia bao la kusawazisha Rovers.

Ndipo ilipotimia dakika ya 87 wakati mwamuzi Mark Clattenburg alijichanganya baada ya kutoa uamuzi kwamba Aaron Hughes alichezewa rafu na Hanley ndani ya sanduku la hatari na Bobby Zamora akaipatia Fulham bao la tatu la ushindi.

Ilikuwa penalti rahisi kufungwa na Zamora, akirejea tena katika Ligi Kuu ya England tangu alipovunjika mguu mwezi wa Septemba.

Nao Everton wakiwa nyuma, walifanikiwa kujipapatua na kuilaza Newcastle 2-1 katika mchezo wa kusisimua sana kwenye uwanja wa Newcastle wa St James Park.

Haki miliki ya picha pa
Image caption Patashika mechi ya Everton na Newcastle

Wenyeji Newcastle walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Leon Best baada ya kuukuta mpira uliokuwa ukizagaazagaa, kutokana na Tim Howard kujichanganya kwa mkwaju uliopigwa na Kevin Nolan.

Leon Osman aliisawazishia Everton kwa mkwaju wa utulivu baada ya kupasiana vizuri na Mikel Arteta.

Na Phil Jagielka aliipatia bao la ushindi Everton baada ya kuunganisha free kick iliyopigwa na Leighton Baines.

Ushindi huo Everton umewafanya wafungane kwa pointi na Newcastle wakiwa na pointi 36, Newcastle wakiwa nafasi ya tisa na Everton ya 10.

Katika mchezo wa awali Birmingham waliporomoshwa nafasi ya hatari ya kushuka daraja, baada ya kukandamizwa mabao 3-1 West Brom, huku James Morrison akifunga bao zuri la pili kwa mkwaju wa mbali uliokwenda moja kwa moja wavuni.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mshikemshike langoni mwa West Brom

Baada ya kipindi cha kwanza kilichopoa, Youssouf Mulumbu alibadilisha hali ya mchezo na kuleta uhai kwa kufunga bao kwa mkwaju wa karibu na lango.

Dakika moja baadae, Jean Beausejour aliisawazishia wenyeji Birmingham baada ya kupokea pasi ya chini ya pembani kutoka kwa Lee Bowyer.

Baada ya Morrison kuachia mkwaju mkali wa kushoto na kuipatia bao la pili West Brom, Paul Scharner aliipatia bao la ushindi kwa kichwa.

Matokeo hayo yameisaidia West Brom nao kujichomoa kutoka mkiani na sasa wapo nafasi ya 16 nyuma ya West Brom.