Joes Mourinho akoswakoswa kuchomwa kisu

Mtu mmoja inaarifiwa alijaribu kumchoma kisu meneja wa Real Madrid, Jose Mourinho wakati alipokuwa akisaini vitabu vya mashabiki kwenye uwanja wa ndege nchini Hispania.

Image caption Jose Mourinho

Mlinzi mmoja wa klabu ya Real Madrid alichomwa kisu na amepata majeraha madogo katika tukio hilo lililotokea uwanja wa ndege wa La Coruna, Galicia, kaskazini mwa Hispania.

Tukio hilo lilitokea siku ya Ijumaa, lakini liliarifiwa hivi karibuni na kituo cha televisheni cha Cadena Ser.

Haijafahamika iwapo Mourinho alikuwa amefahamu juu ya tukio hilo kwa wakati huo.

Cadena Ser kimesema mlinzi huyo hakutanabahi kuwa amechomwa kisu, hadi alipokuwa ndani ya basi la timu.

Hata hivyo kamera za usalama kwenye uwanja wa ndege, huenda zimenasa tukio hilo, kwa mujibu wa kituo hicho cha Cadena Ser.

Kikinukuu chanzo cha habari kutoka Real Madrid, Cadena Ser kimesema klabu hiyo imeimarisha ulinzi kwa timu yake itakapocheza na Racing Santander mwishoni mwa wiki hii.