Kolo Toure alitumia dawa kujikondesha

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger anaamini vipimo vilivyoonesha Kolo Toure anatumia dawa za kumuongezea nguvu ni kutokana na "kutumia dawa za mkewe za kupunguza uzito".

Haki miliki ya picha Getty

Mlinzi huyo wa Manchester City mwenye umri wa miaka, 29, amesimamishwa kucheza soka baada ya vipimo kuonesha anatumia dawa za kuongeza nguvu.

Lakini meneja huyo wa zamani wa Toure, Wenger amezungumza na mchezaji huyo na amesema: "Anataka kudhibiti uzito wa mwili wake kwa kiasi fulani kwa sababu hapo ndipo panamtatiza.

"Anaishi maisha safi kabisa, ni mkweli, mara zote anakuwa nyumbani ni mtu anayejali familia yake."

Toure aliarifiwa na Chama cha Soka cha England, vipimo alivyochukuliwa wakati wa mechi baina ya Manchester United na Manchester City mwezi uliopita, vimeonesha anatumia dawa za kuongeza nguvu.

Shirika la kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu duniani (Wada) imeiorodhesha dawa hiyo "specified substance" kuwa ni moja ya dawa zinazokatazwa kutumiwa na wanamichezo.

Adhabu kwa kosa hilo inaweza kuwa ni onyo ama kufungiwa kucheza kwa miaka miwili.

Baada ya sampuli za vipimo vya Toure kuonesha anatumia dawa hiyo, Manchester City ilithibitisha katika taarifa yake, mchezaji huyo amesimamishwa wakisubiri "matokeo ya mchakato wa kisheria".

Toure ametakiwa hadi siku ya Jumatano, tarehe 9 mwezi huu wa Machi, kuamua iwapo anataka au la kufanyiwa vipimo vingine. Iwapo atakubali na majibu yakionesha hatumii dawa hiyo, basi shauri hilo litakuwa limefungwa na Toure atakuwa hana hatia.

Hata hivyo, iwapo hatakubali kufanyiwa tena vipimo, atatakiwa kuwasilisha maelezo na atakabiliwa na adhabu ya muda mrefu.