Bougherra na Diouf kuadhibiwa zaidi

Wachezaji wawili wa klabu ya Rangers, Madjid Bougherra na El Hadji Diouf, huenda wakaadhibiwa zaidi kufuatia kuoneshwa kadi nyekundu siku ya Jumatano katika mchezo dhidi ya Celtic.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption El Hadji Diouf

Wachezaji hao wawili walioneshwa kadi nyekundu na moja kwa moja watakosa mechi moja ya Kombe la Scotland.

Lakini tabia zao kama zilivyoelezwa katika ripoti ya mwamuzi Calum Murray, huenda wakaongezewa adhabu.

Bougherra aliukamata mkono wa mwamuzi Murray alipokuwa akijaribu kumuonesha kadi nyekundu, wakati Diouf alionesha upinzani na baadae akawarushia fulana mashabiki wa Rangers.

Bougherra mlinzi anayechezea pia timu ya taifa ya Algeria, alitolewa nje kwa kadi nyekundu muda mfupi kabla ya kumalizika mpambano huo wa kuwania Kombe la Scotland, ambapo Rangers walifungwa 1-0 katika mchezo huo wa marudio.

Diouf mshambuliaji wa kimataifa wa Senegal, alioneshwa kadi nyekundu baada ya kupulizwa filimbi ya mwisho.

Kama ilivyo, kufungiwa kwao kutakuwa kwa mechi za Kombe la Scotland msimu ujao, lakini ripoti ya mwamuzi imeonesha kutokea vurugu zaidi na Chama cha Soka cha Scotland huenda kikachukua hatua zaidi.

Lakini kwa mujibu wa BBC nchini Scotland, meneja wa Celtic Neil Lennon na meneja msaidizi wa Rangers Ally McCoist, wanakabiliwa na adhabu ya kufungiwa kutokaa katika benchi la ufundi la timu zao, baada ya kutoleana maneno makali mwisho wa mchezo.

Waliitwa katika chumba cha waamuzi baada ya mchezo huo na wakafahamishwa na mwamuzi wa akiba Iain Brines.

Lennon anakabiliwa na adhabu ya mechi nane na tukio la hivi karibuni ni la pili kuripotiwa msimu huu.

Adhabu yake ya kufungiwa mechi sita ilipunguzwa na kuwa mechi nne baada ya kushinda rufaa yake siku ya Alhamisi.

McCoist anakabiliwa na adhabu ya mechi mbili kwa vile hili ni kosa lake la kwanza.