'Mawaziri waibiwa' Ivory Coast

Haki miliki ya picha AP
Image caption Nyumba za mawaziri zapekuliwa

Vijana na mjeshi ya usalama nchini Ivory Coast yamepekura nyumba za "mawaziri" walioteuliwa na Alassane Ouattara, anayekubalika zaidi kuwa Rais.

Mashariki mwa nchi hiyo, waliokuwa waasi wanaomwuunga mkono Bw Ouattara dhidi ya mpinzani wake, Laurent Gbagbo, wameuteka mji wa Toulepleu.

Ivory Coast imekuwa katika ghasia tangu upigaji kura uliofanyika mwezi Novemba, Bw Gbagbo alipokataa kumkabidhi madaraka Bw Ouattara.

Ghasia hizo zimesababisha kutolewa kwa onyo la kuwepo mgogoro wa kibinadamu kutoka kwa mashirika ya kutoa misaada.

Walioshuhudia huko Abidjan walisema katika siku za hivi karibuni makundi ya vijana yamekuwa yakivamia nyumba za maafisa walio washirika wa Bw Ouattara na kuondoka na mali zao, huku polisi wenye sare zao wakiangalia tu.

Maafisa hao wamekuwa wakikaa na Bw Ouattara wakiwa chini ya Umoja wa Mataifa katika hoteli moja mjini humo.

Wote wawili Bw Ouattara na Bw Gbagbo wametaja majina ya baraza lao la mawaziri- waziri mkuu wa Bw Ouattara ni aliyekuwa kiongozi wa waasi Guillaume Soro.