Maafisa wa Uingereza waachiliwa Libya

Manuwari ya Jeshi la Uingereza
Image caption Manuwari ya Jeshi la Uingereza

Kundi moja la wanadiplomasia wa Uingereza, wakiwemo wanajeshi sita ambao wanaaminika kuwa maafisa wa kijasusi SAS, wameachiliwa huru siku mbili baada ya kuzuiliwa mjini Benghazi, Mashariki mwa Libya.

Maafisa hao wanaaminika kuondoka mjini humo kuelekea nchini Malta wakitumia manuwari ya kijeshi HMS cumberland.

Ripoti zinasema wanajeshi hao walikuwa na mwanadiplomasia mmoja ambaye alikuwa akijaribu kushaurianana viongozi wa upinzani nchini Libya.

Walioshuhudia tukio hilo wanasema maafisa hao walikamatwa na wanajeshi waasi baada ya kuwasili mjini Benghazi, kwa helicopta siku ya Ijumaa iliopita.

kundi hilo lilikamatwa baada ya kuingia ndani ya majengo ya afisi za wizara ya kilimo, wakati maafisa wa ulinzi wa Libya, walipogundua kuwa walikuwa wamebeba silaha, risasi, maguruneti, ramani na hati za kusafiria za raia wa mataifa manne tofauti.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wanajeshi waasi nchini Libya

Walioshuhudia kisa hicho wanasema watu hao walikana kuwa walikuwa na silaha.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, William Haque, amesema, juhudi za wanadiplomasia hao za kushauriana na viongozi wa upinzani nchini Libya kuhusu ghasia zinazoendelea nchini humo zimeshindikana.

Hata hivyo Haque, amesema wamefanikiwa kutatua mzozo ulioibuka kati ya waasi hao na maafisa wake.

Bwana Haque, ameongeza kusema baada ya mashauriano na viongozi wa upinzani nchini Libya, watatuma kundi lingine ili kujaribu kukwamua mazungumzo kati yao.

Wakati huo huo Haque, amekariri kuwa Uingereza bado inaungana na jamii ya kimataifa kumtaka kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi, kuitikia wito wa raia wa nchi hiyo na kuondoka madarakani.