Gbagbo sasa adhibiti mauzo ya Kakao

Zao la Kakao Haki miliki ya picha AP
Image caption Wadadisi wanasema utawala wa Gbagbo hauna pesa za kunua kakao kutoka wakulima

Laurent Gbago ameamuru kuwa serikali yake isimamie mauzo yote ya zao la kakao nchini Ivory Coast na kwenye soko za kimataifa.

Gbagbo ametangaza kauli hiyo kwenye televisheni ya kitaifa, ambapo alisema utawala wake sasa utanunua zao hilo kutoka wakulima wote nchini humo.

Tangazo hili litabdadilisha sana mauzo ya zao kakao. Serikali ndio itakayo nunua zao hilo kutoka kwa wakulima laki saba kote nchini humo, tofauti na mfumo wa soko huru uliopo sasa.

Kwanzia sasa serikali itaamua bei kila msimu wa mavuno. Wadadisi wanasema tangazo hili litavuruga soko la zao hilo na kutakuwepo na faida kidogo sana kwa utawala wa Gbagbo ambao unataka kudhibiti biashara hiyo muhimu.

Hapo awali, Alassane Ouatarra anayetambulika na jumuiya ya kimataifa kuwa ndiye aliyeshinda uchaguzi wa urais nchini humo, alitaka biashara ya kakao isusiwe kwa muda kama njia moja ya kumshinikiza Gbagbo aondoke mamlakani. Kakao inatumika kutengeneza chokoleti, kiburudisho muhimu duniani na Ivory Coast ndio nchi ya tatu duniani kwa kuzalisha zao hilo.

Hata hivyo vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa ulaya vitatatiza sana mauzo ya zao hilo katika nchi za ulaya, ambazo ni soko muhimu la kakao kutoka Ivory Coast.

Mwandishi wa BBC mjini Abidjan, anasema itakuwa vigumu kwa utawala wa Gbagbo kutekeleza amri hii kwa kuwa haina fedha za kuwalipa wakulima, takwimu za wanaozalisha zao hilo na hata ghala za kuhifadhi kakao zitakazo vunwa. Anasema tangazo hilo litachochea zaidi biashara ya magendo kupitia nchi jirani kama vile, Ghana, Togo na Liberia.