Gaddafi ashambulia waasi upya

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ras Lanuf

Majeshi yanayomtii kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi yamezidi kufanya mashambulio ya anga katika eneo la bandari ya mafuta linaloshikiliwa na waasi Ras Lanuf, katika mapigano mapya.

Walioshuhudia walisema ndege za kivita zimeangusha makombora katika maeneo waishio watu na karibu na maeneo waishio waasi.

Hapakuwa na taarifa zozote za mauaji.

Wakati huo huo, msemaji wa waasi alisema mwakilishi wa Kanali Gaddafi alipendekeza kufanya mazungumzo atakapoondoka.

Msemaji huyo alisema, waasi hao walikataa pendekezo hilo.

Mtu mmoja wa upinzani, Jalal al-Gallal, aliiambia BBC: "Kuondoka ni jambo moja, lakini kutoshtakiwa baadae haikubaliki."

'Udhibiti wa kijeshi'

Hakujakuwa na kauli yeyote kutoka serikali ya Kanali Gaddafi kutokana na kauli hiyo ya waasi, lakini kiongozi huyo wa Libya amekataa kuachia madaraka enzi za nyuma.

Anadai hana nafasi yeyote, na hivyo haiwezekani kwake kujiuzulu.

Mwandishi wa BBC Wyre Davies, mjini Tripoli, alisema upande wa Kanali Gaddafi unaamini unazidi kuhodhi eneo kubwa kijeshi, wakidhibiti eneo la magharibi mwa Libya.

Siku ya Jumatatu, majeshi yanayomwuunga mkono Kanali Gaddafi yalidhibiti upya mji wa Bin Jawad, kwenye barabara inayoelekea Ras Lanuf, eneo lililohodhiwa na waasi siku ya Ijumaa.

Kwa kushambulia kwa njia ya anga, helikopta na silaha nzito, waliweza kuwasukuma waasi katika pwani ya kaskazini.

Mwandishi wetu alisema kwa hali hii, ni vigumu kuona uongozi wa Gaddafi ukitaka kuzungumzia suala la kurithiwa.